Na John Walter-Mbulu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara kimehitimisha rasmi kampeni zake za uchaguzi mkuu ngazi ya mkoa leo Wilayani Mbulu, katika viwanja vya CCM vilivyopo Kijiji cha Dongobeshi, kwa mkutano mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama na wapenzi wa chama hicho.
Akifunga kampeni hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, aliwapongeza wagombea wote wa chama hicho kwa kufanya kampeni za kistaarabu, zenye hoja na zisizo na matusi, katika kipindi chote cha kampeni.
“Tofauti na wengine, sisi CCM tumefanya kampeni za hoja na utu. Nitoe wito kwa wananchi wote wa Manyara kujitokeza kwa wingi siku ya Jumatano, Oktoba 29, 2025, kupiga kura kwa amani na kuichagua CCM ili tuendelee na maendeleo,” alisema Toima.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Mbulu, alisema chama hicho kina nafasi kubwa ya kushinda kutokana na vyama vya upinzani kushindwa kuwasimamisha wagombea wanaojitosheleza, hivyo wananchi hawana sababu ya kubadilisha mwelekeo wa maendeleo uliopo sasa.
Emmanuel Nuwas, mgombea ubunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, alieleza mikakati ya utekelezaji wa maendeleo ya wananchi kwa kipindi kijacho cha miaka mitano, akisisitiza kuwa Serikali ya CCM itaendelea kuboresha huduma za jamii na kuinua kipato cha wananchi.
Naye Mhe. Zacharia Issay, mgombea ubunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, aliwataka wapigakura wote kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, akisema kura zao ndizo zitakazoamua mustakabali wa maendeleo ya wilaya hiyo.
Aidha, viongozi hao walisema uchumi wa Mkoa wa Manyara umeimarika, na kwa sasa umepanda hadi kuwa miongoni mwa mikoa kumi bora kiuchumi nchini, ukiwa nafasi ya nane, hivyo ni muhimu wananchi kuendelea kuiamini CCM ili kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.
Mkutano huo wa kufunga kampeni kimkoa uliambatana na shamrashamra, nyimbo za uzalendo na wito wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

0 Maoni