F Mradi wa majiko banifu watambulishwa Hanang,Majiko 1,583 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku | Muungwana BLOG

Mradi wa majiko banifu watambulishwa Hanang,Majiko 1,583 kusambazwa na kuuzwa kwa bei ya ruzuku






Wakazi wa Hanang waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia.

Rai hiyo imetolewa jana November 19,2025 na Mkuu wa Wilaya ya Hanang Almishi Hazali wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku.

"Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika kutunza na kuhifadhi mazingira"amesema Hazali.

Mradi huu unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ni mwendelezo wa  juhudi za serikali  katika kutunza mazingira na kuboresha afya za  wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Aidha Serikali imeweke ruzuku ya asilimia 80 katika  kila jiko  ili kumpunguzia mwananchi hususani wa  maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji gharama ya kununua jiko  na hivyo badala ya mwananchi kununua jiko kwa Tsh 56,000 atanunua kwa  Tsh 11,200 pekee.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Afisa masoko wa kampuni ya L’S Solution ambayo ndio kampuni itakayo sambaza majiko hayo, Ndugu Henry Isack amesema,"Mradi huo unakwenda kubadilisha mtazamo wa wananchi katika matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kutoka kutumia kuni na mkaa mwingi  mpaka kutumia kuni na mkaa kidogo wakati wa kupika".

Aliongeza kuwa majiko haya yametengenezwa kwa nyenzo ambazo zinasaidia jiko kuhifadhi joto kwa mda mrefu hivyo kupunguza matumizi makubwa ya mkaa na kuni

Aidha majiko haya hayatoi moshi na hivyo kupunguza uzalishaji wa  sumu itokanayo na kuni na mkaa ambayo husababisha magonjwa yanayochangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba.

Aidha Hazali, ameishukuru na kuipongeza REA pamoja na mtoa huduma kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa majiko banifu kwa bei nafuu  na yenye ufanisi mkubwa wakati wa utumiaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni