Serikali mkoani Manyara imewaonya viongozi wa umma mkoani humo watakaojaribu kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na ubadhilifu wa majiko banifu yanayopaswa kuwafikia wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ametoa onyo hilo wakati akizindua zoezi la uuzaji na usambazaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa upatikanaji na uhamasisha wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Sendiga amesema mpango huo umelenga kuhakikisha wananchi wote, hususani wa kipato cha chini, wanapata fursa ya kutumia nishati safi na salama ya kupikia kwa gharama nafuu.
Aidha,amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote mkoani Manyara kusimamia kwa makini zoezi hilo, ili kuhakikisha majiko yanauzwa kwa bei iliyoelekezwa ya ruzuku ya kiasi cha TZS 11,200 ambayo ni sawa na asilimia 80 ya ruzuku ya TZS 56,000 na kuepuka udanganyifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza wakati wa zoezi.
“Hatutavumilia udanganyifu na ubadhilifu wowote utakao jitokeza wakati wa zoezi,” amesema Sendiga
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa mkuu wa mkoa, Mhandisi wa miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini, Ramadhani Mganga amesema kwa mkoa wa Manyara mradi unatarajia kugharimu kiasi cha zaidi ya TZS Milioni 354.5 kiasi ambacho kitawezesha usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 7,914 kwa bei ya ruzuku mkoa mzima.
Mhandisi Mganga amesema, wilaya zitakazonufaika na mradi ni wilaya zote tano (5) za mkoa wa Manyara ambazo ni wilaya ya Kiteto, Mbulu, Simanjiro, Hanang na Babati na kila wilaya kupata majiko 1,583 isipokuwa wilaya ya Babati ambayo itapata majiko 1,582.


0 Maoni