F Wapiga Kura 86,400 Jimbo la Mbulu Mjini Waanza Kupiga Kura kwa Utulivu | Muungwana BLOG

Wapiga Kura 86,400 Jimbo la Mbulu Mjini Waanza Kupiga Kura kwa Utulivu


Na John Walter -Mbulu

Wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini, mkoani Manyara, wameanza kupiga kura leo katika vituo 241 vilivyotengwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya zoezi la kupiga kura za madiwani, wabunge na rais.

Zoezi hilo limeanza rasmi saa 1:30 asubuhi, ambapo wananchi wameanza kujitokeza mapema katika vituo mbalimbali kutimiza haki yao ya kikatiba, huku vituo hivyo vikitarajiwa kufungwa saa 10:00 jioni.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Filemon Linus, amesema jumla ya wapiga kura 86,400 wamesajiliwa kushiriki katika uchaguzi huo na maandalizi yote yamekamilika kwa ufanisi.

Amesema kuwa wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa utulivu na amani, huku wakihimizwa kuendelea kujitokeza mapema kabla ya kufungwa kwa vituo.

“Tunawaomba wananchi wote wa Mbulu Mjini wajitokeze mapema kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka. Zoezi linaendelea vizuri na kwa utulivu mkubwa,” alisema Linus.

Aidha, amebainisha kuwa watu wenye mahitaji maalum wamewekewa mazingira rafiki, wakiwemo waliotengewa njia maalum, viti vya magurudumu, na huduma ya kusaidiwa na wasaidizi waliowandaliwa rasmi ili kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika mchakato huo muhimu wa kidemokrasia.

Wananchi waliohojiwa wamesema wamehamasika kushiriki mapema ili kuepuka msongamano na kuhakikisha kura zao zinahesabiwa kwa wakati.

Uchaguzi huo unatarajiwa kumalizika saa 10:00 jioni ambapo zoezi la kuhesabu kura litaanza mara baada ya vituo kufungwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni