Na Timothy Itembe Tarime.
JAMII imetakiwa kujitokeza kwa wingi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa lengo la kujikinga na gharama kubwa za matibabu, huku ikihimizwa kuachana na imani potofu kwamba mtu akijiunga na Bima ya Afya anaweza kufariki kabla ya wakati wake.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, jana wilayani Tarime wakati akizindua Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote lenye kaulimbiu ya “Fursa kwa Makundi Maalumu”, pamoja na mpango wa ujenzi wa Bweni la Wasichana. Kongamano hilo lilifanyika katika Ukumbi wa CMG Hotel na kuwashirikisha viongozi mbalimbali kutoka mikoa tofauti nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Kanali Mtambi alisema gharama za matibabu zimekuwa changamoto kwa familia nyingi, kwani ugonjwa unapomkumba mmoja wa wanafamilia, baadhi hulazimika kutumia mali zao au fedha zote walizonazo kugharamia matibabu, hali inayoweza kuwasababishia umaskini na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na kukosa fedha za matibabu.
“Kama sote tunavyofahamu, suala la matibabu katika familia nyingi, wanapopatwa na magonjwa, huangukia kuwa masikini, hata wengine kupoteza maisha kwa ukosefu wa fedha za matibabu,” alisema Mtambi.
Mtambi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, kwa kuanzisha kongamano hilo, akisema ni hatua muhimu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi na kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote alisema makongamano ya aina hiyo ni miongoni mwa njia muhimu za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya na kuondoa dhana potofu zinazoweza kuwakatisha tamaa wananchi kujiunga na mfuko huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, alisema baadhi ya wananchi wanashindwa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote kutokana na changamoto wanazokutana nazo wanapotaka kupata huduma katika vituo vya afya alisema baadhi ya wanufaika wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma huambiwa kuwa kifurushi walichonacho hakipatikani katika kituo hicho cha afya, hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wengi wanajiunga na Bima ya Afya.
Ghati aliwataka wadau mbalimbali kuunga mkono mkakati huo wa Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa sera ya afya, pamoja na kusaidia ujenzi wa Bweni la Wasichana litakalosaidia kuwawezesha wanafunzi wa kike kusoma katika mazingira salama na kuwaepusha na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri elimu yao.
Naye Afisa wanachama Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mara, Felister Renatus, alisema hadi Agosti 21, 2026, hali ya usajili wa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu bima ya afya katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Mara ilikuwa imefikia usajili wa wanufaika 32,541 dhidi ya lengo la 6,244, huku utekelezaji ukitajwa kuwa asilimia 37.7 katika halmashauri tisa za mkoa huo.
Felister aliongeza kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu mpango huo, pamoja na taarifa kuhusu zoezi la usajili kutowafikia wananchi

