Mvutano Canada na Marekani Wazidi, Ushuru Mpya Waanza Kutekelezwa


Canada imeanza kutekeleza ushuru wa kulipiza kisasi kwa bidhaa mbalimbali kutoka Marekani, huku kukiwa hakuna dalili za nchi hizo mbili kufikia makubaliano ya kibiashara.

Ushuru huo unalenga bidhaa za Marekani zenye thamani ya karibu dola bilioni 20, huku viwango vikifikia asilimia 50. Bidhaa zilizoathiriwa ni pamoja na chuma, vifaa vya elektroniki, bidhaa za kilimo na nguo.

Canada awali pia ilipanga kutoza ushuru kwa baadhi ya bidhaa za baharini, ikiwemo kamba aina ya lobster, lakini ikaondoa bidhaa hizo baada ya wazalishaji wa sekta hiyo nchini kupinga hatua hiyo.

Maafisa wa Marekani na Canada wamesema bado wanataka kufikia makubaliano ya kibiashara, lakini mazungumzo yaliyovunjika mwishoni mwa Agosti hayajaanza tena.

Hatua hiyo inaongeza mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili, huku Canada ikitegemea kwa kiasi kikubwa soko la Marekani kwa mauzo yake ya nje. 

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi