Urusi na Korea Kaskazini zimefungua daraja lao la kwanza la barabara linalounganisha nchi hizo, hatua inayorahisisha usafirishaji wa bidhaa na safari za abiria kuvuka mpaka kwenye Mto Tumen.
Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vimesema daraja hilo litatumika kuwezesha mabadilishano ya wafanyakazi, utalii na biashara.
Hata hivyo, shirika la kijasusi la Ukraine, Truth Hounds, limesema daraja hilo limejengwa zaidi kuwa njia ya siri ya kusafirisha vifaa vya kijeshi kwa ajili ya kuisaidia Urusi katika vita vya Ukraine.
Ufunguzi huo unafanyika wakati uhusiano kati ya Urusi na Korea Kaskazini ukiendelea kuimarika tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine mwaka 2022. Nchi hizo pia zimesaini makubaliano ya kusaidiana kijeshi endapo mmoja wao atakabiliwa na uchokozi.
Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin, amelielezea daraja hilo kuwa “ishara mpya ya urafiki”, huku Waziri Mkuu wa Korea Kaskazini, Pak Thae Song, akilitaja kuwa “tukio la kihistoria.”
Daraja hilo lenye urefu wa takriban kilomita moja lina njia mbili na lina uwezo wa kupitisha hadi magari 300 kwa siku.
