Na Timothy Itembe.
VIONGOZI wa Tanzania Nile Discourse Forum (TNDF), jukwaa linaloshirikisha wadau wa uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kutoka nchi 10 za mradi wa Bonde la Mto Nile, wametembelea Shirika lisilo la Kiserikali la SHIMATA wilayani Tarime, Mkoa wa Mara,kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbadala inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Ziara hiyo imelenga kutathmini utekelezaji wa maarifa na ujuzi uliotolewa kupitia semina, warsha na mikutano mbalimbali kwa taasisi na mashirika yanayofanya kazi katika maeneo ya mazingira, maji na maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa ziara mratibu kanda ya Ziwa(TNDF) Hadija Malimusi, alisema lengo kuu la ziara hiyo ni kujiridhisha namna mafunzo yaliyotolewa yanavyotafsiriwa kuwa miradi halisi inayoweza kusaidia jamii kuongeza kipato huku ikilinda mazingira.
“Tumefika Tarime leo kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa mafunzo na semina zilizokuwa zikitolewa kuhusu uanzishaji wa miradi mbadala ya kiuchumi na kimazingira. Miradi hii inalenga kuisaidia jamii kujikwamua kiuchumi sambamba na kulinda na kuboresha mazingira,” alisema Malimusi.
Malimusi alisema miongoni mwa matokeo ya miradi inayofuatiliwa ni mradi wa sayansi ya jamii wa kupima ubora wa maji katika Mto Mara, ambao ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji.
Alisema kuwa tarehe 6 Oktoba 2026, wanatarajia kuwapokea wajumbe kutoka Benki ya Dunia, ambao watatembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na SHIMATA pamoja taasisi zingine na miradi inayohusiana mafunzo yaliyokuwa yakitolewa.
Kwa upande wake, Asaffa Seyeum, mmoja wa viongozi TNDF), kanda ya Afrika yenye makao mkuu Entebe Uganda aliipongeza SHIMATA kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali, baada ya kutembelea kitalu cha mboga mboga katika Mtaa wa Bugosi pamoja na bustani ya miche ya miti ya matunda, mbao, vivuli na maua katika Mtaa wa National Housing.
Seyeum alisema miradi hiyo inaonyesha namna juhudi za jamii zinavyoweza kuunganisha uhifadhi wa mazingira na shughuli za kiuchumi.
Akisoma risala, Yulitha Constantine Mhado, Mratibu wa Miradi ya Mazingira na Uchumi wa SHIMATA, alisema shirika hilo linatekeleza miradi miwili mikuu inayolenga kuwawezesha wanawake na wasichana pamoja na kuongeza uhifadhi wa mazingira,alisema mradi wa kwanza unahusu kilimo cha mboga mboga kwa wanawake na wasichana, ukiwa na lengo la kuwawezesha kuzalisha kwa ajili ya kuuza na kujikwamua kiuchumi.
Kwa mujibu wa Yulitha, mradi huo pia unalenga kuwasaidia baadhi ya wasichana kupata chanzo cha kipato ili kupunguza utegemezi wa shughuli zinazoweza kuwaweka katika mazingira hatarishi,Mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya takribani Sh milioni 1.94.
Mradi wa pili unahusu upandaji na uzalishaji wa miche ya miti ya matunda, mbao, vivuli na maua, ambapo SHIMATA imezalisha miche 751,000. Mradi huo umegharimu takribani Sh milioni 17.364, fedha ambazo zimetokana na mapato ya ndani aliongeza kusema.
SHIMATA inahitaji takribani Sh milioni 35.07 kutoka kwa wadau wa mazingira na maendeleo pamoja na wadau wa Nile Basin Discourse (NBD) na washirika kusaidia kupata ufadhili kupitia Benki ya Dunia kwa ajili ya kupanua miradi hiyokwa ajili ya ununuzi wa eneo litakalotumika kwa kilimo cha mboga mboga na uzalishaji wa miche ya matunda.
Akizungumza kuhusu changamoto zinazokabili utekelezaji wa miradi hiyo, Mratibu wa SHIMATA, Enanuel Buchafwe, alisema uelewa mdogo wa baadhi ya wanajamii kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri juhudi za uhifadhi.
Alitaja pia mila na desturi zinazokinzana na juhudi za uhifadhi, uhaba wa vitendea kazi na rasilimali za kifedha, pamoja na ukosefu wa maeneo makubwa kwa ajili ya upanuzi wa miradi.
Buchafwe alisema changamoto nyingine ni ufugaji holela wa mifugo mijini bila kuzingatia kanuni na ushauri wa wataalamu, pamoja na kilimo kisichozingatia kanuni bora za kilimo na uhifadhi wa mazingira na kuwa kushughulikia changamoto hizo kunahitaji ushirikiano kati ya jamii, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha miradi ya uhifadhi na uwezeshaji wa kiuchumi inakuwa endelevu.
Ziara hiyo ya TNDF imekuja wakati ambapo juhudi za kuunganisha uhifadhi wa vyanzo vya maji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uwezeshaji wa kiuchumi wa jamii zinaendelea kupewa kipaumbele katika maeneo yanayohusiana na Bonde la Mto Nile.
,,,,,,mwisho,,,,


