MKURUGENZI WA KAMPUNI KEPI AHIMIZA UTUMIAJI WA LISHE ASILIA NA KILIMO HAI KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA.

 


Na Rebeca Duwe Tanga 

 

​ KATIKA jitihada za kuhamasisha jamii kurejea kwenye mfumo wa maisha na ulaji wa vyakula vya asili, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilimanjaro field and Class of environment protection initiative ( KEPI) Elibahati Kimaro, ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na matumizi yaliyokithiri ya kemikali na badala yake wakumbatie kilimo hai na matumizi ya unga wa asili ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.


​Akizungumza wakati wa maonyesho ya miundombinu ya uzalishaji wa unga na mbolea ya asili, Kimaro alieleza kuwa mchakato wa utengenezaji wa bidhaa hizo unazingatia matumizi ya malighafi asilia kutoka shambani na sokoni bila kuongeza kemikali yoyote inayoweza kuhatarisha afya ya mlaji.  


​"Sisi ni wazalishaji wa mbolea na unga wa asili, Mbolea na unga huu unatokana na mchanganyiko wa malighafi mbalimbali za shambani na sokoni, ikiwemo mazao ya nafaka na mbegu za asili za zamani kama mahindi ya rangi mbalimbali na maharagwe," alieleza Kimaro wakati akifafanua hatua za uandaaji wa bidhaa hizo. 

 

​Kimaro amesema kuwa matumizi ya unga huo wa lishe asilia ambao unaweza kutumika kupikia uji au ugali yana manufaa makubwa kwa afya ya makundi yote katika jamii, kuanzia watoto, vijana hadi wazee, kwa kuwa unasaidia kujenga kinga ya mwili na kuongeza nguvu za uzalishaji. 

 

​Akiunganisha matumizi ya lishe hiyo na umri wa kuishi, Mkurugenzi huyo alikumbusha kuwa mababu wa zamani walimudu kuishi miaka mingi kwa afya njema kutokana na kula vyakula visivyo na kemikali, tofauti na sasa ambapo watu wengi huanza kukabiliwa na changamoto za kiafya wakiwa bado katika umri mdogo.

  

​"Wazee wetu waliweza kuishi miaka 100 au zaidi kwa sababu ya kula vyakula visivyo na kemikali nyingi, Sasa hivi mtu akifikisha miaka 70 tayari anakuwa na wakati mgumu kiafya, Tukirejea kwenye vyakula vya asili ambavyo havijatoweka, tutatengeneza miili yetu na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza," alisisitiza Kimaro.

  

​Sambamba na lishe, alitoa wito kwa wakulima na jamii kwa ujumla kutumia mbolea za asili katika uzalishaji wa mazao yao ili kulinda rutuba ya udongo na kuhakikisha chakula kinachofika mezani ni salama kwa afya ya mlaji.


mwisho.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi