WAWEKEZAJI WAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KILIMO NA VIWANDA MUHEZA



Na Rebeca Duwe Tanga


Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga imewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na biashara, ikiwemo kuwekeza katika uzalishaji wa mazao ya kisasa na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani ya bidhaa za wakulima na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.


Muheza ni miongoni mwa maeneo yenye ardhi yenye rutuba inayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara, hali inayoiweka wilaya hiyo katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira pamoja na kipato kwa wananchi.


Akizungumza kufuatia ushindi wa kitaifa uliopatikana katika Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Naima Chondo, amesema wilaya hiyo ina fursa nyingi zinazoweza kutumiwa na wawekezaji katika kuendeleza sekta ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wakulima.


Chondo amewahimiza wawekezaji kutumia fursa hizo kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa pamoja na kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao, hatua itakayosaidia kupanua masoko, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuongeza kipato kwa wakulima.


Amesema uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ni muhimu katika kukuza uchumi wa eneo hilo, kwani utasaidia kuunganisha uzalishaji wa shambani na mahitaji ya soko, huku ukifungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara na wananchi.


Akizungumzia siri ya ushindi walioupata katika maonesho hayo, Chondo amesema maandalizi mazuri na juhudi za kuwawezesha wakulima wadogo kushiriki zimechangia mafanikio hayo. Ameeleza kuwa maonesho hayo yamewapa wakulima nafasi ya kujifunza teknolojia mpya za kilimo, kubadilishana uzoefu na kuonesha ubora wa mazao wanayozalisha.


Ameongeza kuwa maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao, kuanzia uzalishaji shambani hadi kuyafikisha kwa walaji kupitia masoko mbalimbali.


Kwa upande wake, Dastan Dafa, mkulima kutoka Kata ya Amani wilayani Muheza, ameishukuru Serikali kwa kuandaa fursa zinazowawezesha wakulima kupata ujuzi na maarifa mapya yatakayosaidia kuboresha shughuli zao za kilimo.


Dafa amesema ushiriki wake katika maonesho hayo umempa nafasi ya kujifunza mbinu mpya za uzalishaji zitakazomwezesha kuongeza tija, kuboresha ubora wa mazao na kuongeza thamani ya bidhaa anazozalisha.


Amezitaja baadhi ya fursa za kilimo zilizopo Muheza kuwa ni uzalishaji wa mahindi, ndizi na mazao ya viungo kama karafuu, iliki na mdalasini, akieleza kuwa mazao hayo yana uwezo wa kutoa manufaa makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara kupitia masoko ya ndani na nje ya nchi.


Amesisitiza kuwa matumizi ya mbinu bora za kilimo, pamoja na upatikanaji wa masoko ya uhakika na uwekezaji katika uchakataji wa mazao, ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia wakulima kunufaika zaidi na shughuli zao.


Kwa ujumla, fursa zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza zinatoa nafasi kwa wawekezaji kushirikiana na wakulima katika kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kupanua wigo wa masoko. Uwekezaji huo unaweza kuwa chachu ya kukuza uchumi wa wilaya, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi