Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Festo Richard Shirima amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 17 katika Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.
Shirima alikamatwa Mei 6, 2026, majira ya saa 11:50 jioni katika eneo la Kiboro, Kijiji cha Kelamfua, Kata ya Kelamfua Mokala, Tarafa ya Mkuu, Wilaya ya Rombo, akiwa na bunda 33 za majani ya mirungi zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya mfuko wa salfeti, pamoja na mabegi madogo mawili.
Baada ya kukamatwa, alifikishwa mahakamani Agosti 18, 2026, na shauri lake kusikilizwa hadi Oktoba 29, 2026, ambapo alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa mujibu wa kifungu cha sheria 16(1) na 2(c) cha sheria ya kudhibiti wa dawa za kulevya sura ya 95 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2023.
Hukumu hiyo inaonesha hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
