TARI YATAJA TEKNOLOJIA ZA KILIMO ZINAZOONGEZA THAMANI YA MAZAO

 



Na Rebeca Duwe, Tanga


Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeendelea kufanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo zinazolenga kuongeza uzalishaji wa chakula na thamani ya mazao nchini.



Hayo yamesemwa na Mtafiti wa TARI, Gaspar Mgimiliko, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la taasisi hiyo kwenye maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.


Mgimiliko amewahimiza wananchi wanaoshiriki maadhimisho hayo kutembelea banda la TARI ili kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa chakula na uchakataji wa mazao.


Amesema kuwa katika maonesho hayo, taasisi hiyo imeonesha teknolojia mbalimbali, zikiwemo za mbegu bora na uchakataji wa mazao ili kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuziuza sokoni.


Ameeleza kuwa kuongeza thamani ya mazao kunaweza kuongeza mapato ya wakulima na wafanyabiashara, akitolea mfano wa bidhaa ambazo bei yake inaweza kuongezeka kutoka Shilingi 10,000 hadi Shilingi 32,000 baada ya kufanyiwa uchakataji.


Mgimiliko ametaja baadhi ya mazao ambayo yameongezwa thamani kuwa ni korosho, mabibo, ufuta na karanga. Pia, amesema viungo kama mdalasini na iliki vinaweza kuchakatwa na kuongezwa thamani ili kutengeneza bidhaa mbalimbali.


Ameongeza kuwa kupitia teknolojia hizo, wameweza kutengeneza siagi inayotokana na korosho na karanga, juisi ya bibo pamoja na mvinyo unaotokana na tunda hilo.


Amesema teknolojia zinazooneshwa katika banda hilo zimetokana na tafiti zinazofanyika katika vituo mbalimbali vya TARI vilivyopo nchini, kwa lengo la kuwapatia wananchi maarifa na teknolojia zitakazosaidia kuboresha uzalishaji wa kilimo.


“Teknolojia hizi zinatokana na tafiti zinazofanyika katika vituo vyetu vilivyopo nchi nzima. Tumeleta pia mbegu bora zilizopatikana kupitia tafiti hizo, hivyo wananchi wanapaswa kufika kujifunza na kufahamu teknolojia zinazotolewa na taasisi yetu,” alisema Mgimiliko.


Aidha, alisema TARI inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia za kilimo pamoja na kuwapatia taarifa kuhusu mbegu bora za mazao ya chakula, hatua inayolenga kuongeza tija katika uzalishaji.


Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yalianza mwaka 1981, yakiwa na lengo la kuhamasisha mijadala na juhudi mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa chakula na kuendeleza sekta ya chakula duniani.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi