TOAM YAHIMIZA MATUMIZI YA PEMBEJEO ZA KILIMO IKIOLOJIA HAI KWA AFYA BORA YA WATANZANIA

 


Na Rebeca Duwe, Tanga


TANGA — Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga na mikoa jirani wametakiwa kujifunza na kutumia teknolojia za kilimo ikolojia hai, ikiwemo matumizi ya mbolea, viuatilifu na mbegu za asili, ili kulinda afya ya walaji, kuhifadhi rutuba ya udongo na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.


Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula yanayofanyika kitaifa jijini Tanga, ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wanatumia maonesho hayo kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kilimo kinachozingatia afya ya binadamu na mazingira.



Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la kilimo ikolojia hai la Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), Meneja wa Programu wa taasisi hiyo, Paul Chilewa, alisema banda hilo linaonesha bidhaa mbalimbali zinazohusiana na kilimo hai, zikiwemo mbolea, viuatilifu, mbegu za asili na bidhaa zinazozalishwa kwa kuzingatia mnyororo wa thamani wa kilimo hai.


Alisema bidhaa hizo huzalishwa kwa kufuata misingi na viwango vya kilimo hai vinavyolenga kulinda afya ya binadamu na mazingira, huku zikitoa fursa kwa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kufikia masoko yenye mahitaji ya bidhaa zinazozalishwa kwa kuzingatia viwango vya kilimo hai.


Chilewa aliongeza kuwa TOAM, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Wizara ya Kilimo, inatekeleza mkakati wa kilimo ikolojia hai wa mwaka 2023 hadi 2030, unaolenga kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo zinazozingatia misingi ya kilimo hai.


Alisema moja ya vipaumbele vya mkakati huo ni kuwawezesha wakulima kupata mbolea hai, viuatilifu vinavyokubalika katika mifumo ya kilimo hai na mbegu za wakulima, ili kuimarisha uzalishaji endelevu na kupunguza utegemezi wa pembejeo zinazoweza kuathiri mazingira endapo zitatumiwa vibaya.


Akizungumzia umuhimu wa pembejeo hizo kwa wakulima wa Tanga, Chilewa alisema matumizi ya bidhaa zinazofaa katika kilimo hai ni muhimu, hususan kwa wakulima wa matunda na mazao mengine yanayohitaji uangalizi wa karibu katika matumizi ya viuatilifu.


Alieleza kuwa matumizi yasiyofaa ya baadhi ya kemikali za kilimo yanaweza kusababisha mabaki kwenye mazao na kuathiri mazingira, hivyo akasisitiza umuhimu wa wakulima kufuata maelekezo ya matumizi ya pembejeo na kuchagua bidhaa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.


Aidha, alisema soko la kimataifa, ikiwemo baadhi ya masoko ya Ulaya, lina mahitaji ya bidhaa zinazozalishwa kwa kuzingatia viwango vya usalama na ubora. Hivyo, wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni za uzalishaji ili kuongeza fursa za kupata masoko hayo.


Alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya pembejeo zinazokubalika katika kilimo hai yanaweza kusaidia kulinda afya ya walaji, kuhifadhi mazingira na kuchangia ustawi wa wakulima.


MBolea YA MIAMBA YAONESHA FURSA KATIKA KUBORESHA RUTUBA YA UDONGO


Kwa upande wake, Donald Mwakamele, aliyekuwa akionesha bidhaa katika banda la kilimo ikolojia hai, alieleza kuhusu mbolea inayotokana na miamba na ambayo, kwa mujibu wake, inalenga kuboresha rutuba ya udongo kwa kutumia virutubisho vya asili.


Mwakamele alisema bidhaa hiyo hutengenezwa kutokana na miamba yenye madini na virutubisho vinavyoweza kusaidia kuboresha hali ya udongo na kuongeza uwezo wake wa kustawisha mazao.


Alieleza kuwa kiwanda kinachozalisha mbolea hiyo kinapatikana mkoani Songwe na kwamba bidhaa hiyo imeonesha matokeo mazuri katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Njombe, Songwe, Mbeya na Moshi mkoani Kilimanjaro.


Aliongeza kuwa matumizi ya mbolea zinazolenga kuboresha rutuba ya udongo ni sehemu muhimu ya juhudi za kuendeleza kilimo endelevu, hasa pale zinapotumiwa kwa kuzingatia mahitaji ya udongo na aina ya zao husika.


Maonesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wakulima, wataalamu, wazalishaji wa pembejeo na wadau wengine wa sekta ya kilimo, kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazoweza kuchangia uzalishaji endelevu wa chakula na ustawi wa jamii.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi