Na John Walter-Babati
Hatimaye mkazi wa Kijiji cha Magara, Kata ya Magara, Wilaya ya Babati, Loema
Petro, amekabidhiwa eneo lake la ardhi baada ya kulalamika kuporwa eneo hilo
kwa madai ya kughushi nyaraka za umiliki.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, kupokea
malalamiko ya mama huyo wakati wa ziara yake katika Kata ya Magara Oktoba 23,
2026, ambapo alieleza namna alivyopoteza sehemu ya ardhi aliyokuwa ameuza kwa
mtu aliyefahamika kwa jina la Yohana Tluway.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Loema alimuuzia Yohana robo ekari kwa
shilingi laki moja na nusu mwaka 2012, lakini mwaka 2014, Yohana akishirikiana
na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Korongo la Nyani wakati huo, wanadaiwa
kughushi nyaraka na kuonyesha kuwa alinunua ekari moja badala ya robo ekari.
Akifuatilia malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Hashimu Mgandilwa,
alimtafuta Yohana, mkazi wa Kijiji cha Qatesh, Kata ya Gehandu, Wilaya ya
Mbulu, na kumhoji kuhusu tuhuma hizo, ambapo alikiri kughushi nyaraka hizo,
akaomba msamaha na kukubali kurejesha eneo hilo kwa mwenyewe.
Mkuu wa wilaya ameelekeza Yohana kufikishwa polisi kutoa maelezo kuhusu nyaraka
hizo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mgandilwa amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa
kufanya shughuli halali na kumiliki mali kwa njia zinazotambuliwa kisheria,
akionya kuwa vitendo vya kuwadhulumu wengine havitavumiliwa na wote
watakaobainika kujihusisha navyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Amesema vitendo vya aina hiyo ni miongoni mwa vyanzo vya migogoro katika jamii,
akisisitiza kuwa kughushi nyaraka za umiliki wa ardhi ni kosa la wizi
linalopaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
