Na John Walter-Babati
Jimbo la Babati Vijijini limetumia jumla ya Shilingi bilioni
2.2 katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha robo
ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba 2026.
Taarifa iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini
ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Daniel Sillo, inaeleza kuwa katika kipindi hicho Halmashauri ya
Wilaya ya Babati imepokea Shilingi bilioni 1.66 kutoka Serikali Kuu, huku
Shilingi milioni 566.5 zikitokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fedha hizo zimeelekezwa katika
sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, mifugo, uwezeshaji wa wanawake na vijana
pamoja na kuboresha miundombinu ya halmashauri.
Katika sekta ya elimu, Shilingi milioni 543.5 zimetumika
katika ujenzi na ukamilishaji wa madarasa katika shule za msingi na sekondari,
ujenzi wa vyoo pamoja na maabara za shule za sekondari.
Miradi hiyo inahusisha shule za msingi Ayamohe, Ayatlaa,
Gabadaw, Hewasi, Kirusix na Bubu, huku shule za sekondari Qash, Boay, Chief
Dodo, Umagi na Kakoi zikinufaika na ujenzi wa madarasa. Aidha, ujenzi wa vyoo
umefanyika katika shule za msingi Bulkeri na Orbesh, pamoja na ukamilishaji wa
vyoo katika shule ya msingi Ufana.
Katika sekta ya afya, jumla ya Shilingi milioni 883.6
zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa zahanati za Masware na Ngoley, ujenzi na
ukarabati wa Hospitali ya Wilaya, ununuzi wa vifaa tiba kwa Zahanati ya
Endagile pamoja na kuchangia huduma za M-MAMA.
Kwa upande wa mifugo, Shilingi milioni 17 zimetumika
kukamilisha majosho katika vijiji vya Arri na Orbesh, huku Shilingi milioni
126.07 zikitolewa kama mikopo kwa wanawake na vijana kupitia mapato ya ndani ya
halmashauri.
Aidha, katika kuboresha miundombinu ya kiutawala, Shilingi
milioni 638.4 zimeelekezwa katika ukamilishaji wa nyumba ya Mkurugenzi wa
Halmashauri na nyumba za wakuu wa idara.
Taarifa hiyo pia inaonesha kuwa Shilingi milioni 20
zimetumika kwa ununuzi wa vishkwambi kwa ajili ya watendaji wa kata pamoja na
mizani 10 ya kupimia mazao.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Daniel Sillo amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia
Jimbo la Babati Vijijini fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Aidha, amemshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Babati, Mheshimiwa John Silvin Noya, madiwani wote pamoja na Mkurugenzi wa
Halmashauri kwa kuendelea kusimamia ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani
ya halmashauri, ambayo yamechangia kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza huduma za
kijamii na kuboresha miundombinu katika Jimbo la Babati Vijijini kupitia
rasilimali zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya
halmashauri.
