TEMESA KUPAMBANA NA MAGARI YA SERIKALI YANAYOTENGENEZWA NJE YA MFUMO WAKE

 


Na Rebeca Duwe, Tanga


WAKALA wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Tanga umeandaa operesheni maalumu ya kubaini taasisi za serikali zinazofanya matengenezo ya magari yake nje ya mfumo rasmi wa wakala huo, hatua inayolenga kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.


Meneja wa TEMESA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Riziki Lukali, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni, akieleza kuwa zaidi ya magari 200 ya taasisi mbalimbali za serikali yamesajiliwa kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo, lakini idadi ya magari yanayopelekwa kupata huduma hiyo ni ndogo.


Alisema hali hiyo inaibua haja ya kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa utaratibu uliowekwa, ili kuhakikisha taasisi zote za serikali zinatumia huduma za TEMESA kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.


Aliongeza kuwa Mkoa wa Tanga una shughuli nyingi za kiuchumi na kiutawala, hivyo ni muhimu kwa taasisi za serikali kuhakikisha magari yake yanapata matengenezo kupitia mfumo rasmi ili kuongeza mapato ya serikali na kuimarisha utoaji wa huduma.


Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa, Lukali alisema TEMESA imepanga kufanya operesheni maalumu itakayolenga kubaini taasisi zinazokiuka utaratibu huo kwa kupeleka magari yao kutengenezwa nje ya mfumo wa wakala huo bila vibali husika.


Alisema operesheni hiyo pia itasaidia kubaini sababu zinazochangia taasisi hizo kutotumia mfumo wa TEMESA kama inavyotakiwa.


Aidha, alieleza kuwa kuna karakana zilizothibitishwa na kupewa mamlaka ya kutengeneza magari ya taasisi za serikali kutokana na ubora wa vifaa na huduma zake, zikiwemo Lal Garage, Adams Motor na Toyota.


Katika hatua nyingine, TEMESA imetoa onyo kwa karakana zitakazobainika kupokea magari ya serikali bila vibali halali au kutumia vibali vya kughushi, ikisisitiza kuwa haitasita kuzifutia vibali vya kuhudumia magari ya taasisi za serikali.


Hatua hiyo inalenga kuhakikisha matengenezo ya magari ya serikali yanafanyika kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na kulinda mapato ya umma.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi