JESHI la polisi mkoa wa Dodoma linamshikilia Mgombea Ubunge kwa
tiketi ya Chadema, Benson Kigaila pamoja na wenzake kumi ambao ni wafuasi wa
chama hicho.
Kauli hiyo ya kukamatwa kwa wafuasi hao pamoja na mgombea
ubunge huyo ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma , Kamishna Msaidizi, David Misime
alipokuwa akizungumza waandishi wa habari.
Misime alisema Kigaila na wenzake kumi wanadaiwa kukamatwa
kutokana na kufanya maandamano bila kibali na kuzuia watumiaji wengine wa
barabara kushindwa kuendelea na shughuli zao.
Mbali na kufanya maandamano bila kibali jeshi la polisi
linadai kuwa wafuasi wa Chadema walimshambulia askali polisi kwa kutumia chupa
ya soda kumpiga nayo kichwani sambamba na kufanya fujo kituoni.
Misime alisema matukio hayo yalitokea juzi majira ya saa
12:45 kutokea barabara ya Jamatini na kituo cha polisi baada ya mgombea ubunge
wa chadema kumaliza mkutano wake wa kampeni katika eneo la stendi kuu ya Dodoma .
Misime aliwataja waliokamatwa kuwa ni Benson Kigaila mgombea
ubunge Chadema, Khadija Maula, Godfrey Manyanya mwenyekiti BAVICHA mkoa wa Dodoma .
Wengine ni Stellah Masawe, Hashimu Kilaini, Alex Thomasi,
Prisca Mgaza, Luckyson kweka, Aisha Urio, Pompey Remijo na Lawi Tumuza.
Kamanda alisema kuwa watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi
wanaandaliwa jarada kwa ajili ya kuwapandisha kizimbani leo.
Kutokana na hali hiyo kamanda Misime alisema kuwa jeshi
litaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua wanasiasa ambao watafanya kampeni
zao ambazo ni za kuvunja amani.
Hata hivyo Misime hakuweza kumtaja jina askari aliyedaiwa
kujeruhiwa na chupa kichwani na wala hakutaka waadishi wakutane na askari huyo.
