BAADHI ya wakazi wa mji wa Dodoma
wameeleza masikitiko yao
juu ya matusi na kashifa zinazotolewa na viongozi wa CCM dhidi ya wahasimu wao
Chadema.
Hali hiyo ilijitokeza juzi ambapo Makongoro Nyerere aliweka
sera za CCM pembeni na kuanza kutoa kashfa kwa wagombea wa vyama vya siasa
hususani Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa na mgombea Ubunge Benson
Kigaila.
Akihutubia katika mkutano wa Kampeni wa mgombea ubunge CCM
katika viwanja vya Kikuyu Kusini, Makongoro badala ya kutangaza sera za chama
chake alianza kwa kashfa na kudai Ikulu hakuna makabuli hivyo Lowassa anaumwa
na kuna uwezekano akafia Ikulu.
Makongoro akimnadi Anthon Mavunde, alitumia muda mwingi
kutoa kashfa kwa wagombea wa UKAWA huku akidai Lowassa asichaguliwe kuwa rais
kwani afya yake mbaya hivyo anaweza kutofanya majukumu yake.
Mbali na hilo
amesema Ikulu siyo wodi ya wagonjwa na sehemu ya makaburi hivyo ni vyema mtu
anayetakiwa kwenda Ikulu ni mtu mwenye nguvu.
“Mimi sasa sitaki
kuendelea kumsema Lowassa maana akifa watasema mimi ndiye niliyemuua hata hivyo
nawashangaa watu wa UKAWA wana roho ngumu sana
kutembea na mtu ambaye amechoka vile.
“Chadema wanatakiwa
kushitakiwa ni maajabu sana kuona na watu
wasivyo na huruma wanamtesa sana
baba wa watu hata hawezi kuzungumza majukwaani na sera anamwachia Lissu
(Tundu),” amesema Makongoro.
Kutokana na hali hiyo wakazi wa Dodoma wamesema watanzania wanataka
kusikiliza sera na siyo vinginevyo.
Mmoja wa wananchi wa Kikuyu Kaskazini ambaye alijitambulisha
kuwa ni kada wa CCM na kukataa jina lake
litajwe alisema ana
mashaka na wana CCM huenda wana mpango wa kuua chama.
Alisema haiwezekani viongozi wa CCM badala ya kutangaza sera
wao wanajielekeza katika matusi na kashifa,mambo ya afya ya mtu anaijua Mungu
mwenyewe.
