Jana ilikuwa ni
Septemba 26 ambapo UKAWA waliendelea na mikutano yao
ya kampeni za kuomba
ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi .Jana ilikuwa
ni zamu ya wakazi wa Wilaya ya Hai ambapo Waziri
Mkuu wa zamani, Fredrik Sumaye aliendelea na kazi ya
kupangua mashambulizi ya CCM.
Sumaye aliitumia siku ya jana kumjibu Dk Magufuli aliyesema
kuwa utafiti uliofanywa na Twaweza unaoonyesha anaongoza kwa asilimia 65,
umempunja ushindi aliostahili.
Akizungumza katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika
Rundugai, Jimbo la Hai, Sumaye alisema Dk Magufuli amekuwa akikisahau hata
chama chake na kuwataka wananchi wachague Tanzania
ya Magufuli, huku akiomba wananchi wasichome godoro lote lenye kunguni badala
yake waue kunguni waliopo kwenye godoro hilo .
“Haiwezekani mkalalia
kitanda chenye kunguni si ndiyo,” alihoji Sumaye na kuitikiwa na wananchi “ndiyoooooo”.
“Amesahau hata kusema
chagua CCM, anasema chagua Tanzania ya Magufuli,” alisema Sumaye na
kuongeza kuwa Tanzania
haiwezi kuwa ya Magufuli, bali ni ya Watanzania wote.
Sumaye alisema kuwa hali ya CCM ni mbaya na ndiyo maana
wananchi wamechoka na hali zao ni mbaya.
“Wananchi wanataka
mabadiliko, hakuna vita itakayotokea kama wanavyohubiri huo ni upuuzi mtupu,”
alisema Sumaye.
Sumaye aliwaambia wananchi hao wa Rundugai kuwa nchi nyingi
duniani zinapata mabadiliko kwa kubadilisha mfumo uliopo, hivyo wananchi
wasiogope kwa kuwa CCM siyo mama yao ,
bali ni chama cha siasa.
Lowassa Aahidi Kudhibiti
Rushwa Ndani Ya
Siku 100
Wakati Sumaye akisema hayo ,mgombea urais kwa tiketi ya
Chadema, Edward Lowassa aliahidi
kuhakikisha anapambana na tatizo la
rushwa ambalo limekuwa chanzo cha umasikini nchini.
"Siku 100 za
serikali ya Chadema, tutaunda chombo kila wilaya ambacho kitakuwa ‘one stop
centre’. Ukienda mjini kwa shughuli za kiserikali huduma zote zitakuwa sehemu
moja, hii itaondoa urasimu na rushwa." Alisema Lowassa.
Huku akionekana kujiamini kushinda katika chaguzi
ujayo,Lowasa alisema atahakikisha anaongoza nchi kwa misingi ya haki na usawa
huku akiahidi kutumia vema ilani ya ukawa kuhakikisha anapambana na rushwa.
Alisema kwa mara ya kwanza nchini Tanzania upinzani
utachukua nchi na akasisitiza
kuwa CCM lazima
Ing'oke mwaka huu.
"CCM lazima ing'atuke
mwaka huu, lakini itang'atuka
kwa kura zenu, hivyo
nawaombeni mtunze sana
vichinjio vyenu."
Alisema Lowassa na
kuongeza;
“Wale wenzangu
waliochukia mimi kuondoka CCM, sasa wameanza kukubali uamuzi wangu kwa kuwa CCM
imeshindwa kuongoza nchi, haifai tena kuongoza kama Sumaye alivyosema.Hali ya wananchi
ni mbaya sana ."
Lowassa aliendelea kurudia ahadi zake za elimu bure kuanzia
msingi hadi chuo kikuu, pia kuboresha maisha ya Watanzania waondokane na
umaskini ambao kila siku amekuwa akisema anauchukia.
Katika mkutano huo, Lowassa alimsihi Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe kuendelea kuambatana naye kwenye kampeni ili aongeze nguvu kwenye
timu yake.
Lowassa alisema Mbowe anaweza kufanya kampeni zake kwenye
Jimbo la Hai na kuweka timu ambayo itamsaidia wakati atakapokuwa nje ya jimbo
kumpigia kampeni mgombea urais.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbowe aliiponda CCM akisema
kwa sasa haijielewi kwa kuwa iko hoi.
Alisema katika uchaguzi huu hawatakubali kuibiwa kura huku
akiwaomba askari wakae pembeni ya siasa na kulinda amani ili wanasiasa wacheze
ngoma yao
wenyewe.
“Askari wetu lindeni
amani tuachieni CCM tucheze nao msipendelee upande wowote,” alisema Mbowe.
