RAIS UHURU KENYATTA.
Tarehe 8 Agosti mwaka huu Wakenya watatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wapya akiwamo rais. Wanasiasa, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC) na wananchi wanaendelea kujiandaa kwa ajili hiyo.
Kadri siku zinavyozidi kusonga joto la uchaguzi huo linazidi kupanda, na hivi sasa wanasiasa wameanza kujisogeza sogeza karibu na wananchi kwa kutoa maneno matamu.
Rais Uhuru Kenyatta aliyeingia kwa mara ya kwanza Ikulu mwaka 2012 ameanza kuwapa Wakenya maneno matamu ya kuwalainisha ili mwezi Agosti wampe muhula wa pili ambao ni wa mwisho kwake.
Mzozo wa madaktari ulioanza mwezi Desemba mwaka jana unaonekana kuanza kumpa kiwewe Kenyatta kwa kuamini kuwa athari zilizotokana na mgomo huo zinaweza kumwangukia yeye kwenye uchaguzi huo.
Ingawa mwenyewe amekaririwa mara kadhaa huko nyuma kwamba hababaishwi na mgomo huo, lakini kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia, Kenyatta amekuwa akitoa maneno matamu matamu kwa Wakenya.
Moja ya kauli zinazoashiria kuwa Rais Kenyatta ameanza kuonja joto la Uchaguzi Mkuu wa Agosti ni ile aliyoitoa wiki iliyopita ya kutaka kupunguzwa mishahara ya wabunge na maafisa wakuu akisema suala hilo limechangia kuzuka kwa migomo ya wafanyakazi.
Rais Kenyatta aliyasema hayo alipohutubia kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza uongozini na kuongeza kuwa viwango vya juu vya mishahara ya wabunge vimesababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine kutaka nyongeza za mishahara.
Hotuba ya Kenyetta ilisheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na upinzani kila uchao kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota kwa huduma za afya, elimu na usalama.
Kwenye mkutano huo, Uhuru alijivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya magaidi nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za kimataifa cha asilimia tatu kwa mwaka.
Rais Uhuru alitaja mmoja baada ya mwingine miradi ambayo serikali yake imetimiza katika kipindi cha miaka minne uongozini.
Lakini pamoja na yote kauli iliyoibua hisia ni ile ya kutaka mishahara ya wabunge na maafisa wakuu wa serikali ipunguzwa.
Mishahara ya vigogo ipunguzwe
Kauli ambayo ilitafsiriwa kama janja yake ya kampeni, Uhuru alisema viwango vya juu vya mishahara ya wabunbe vimewafanya wafanyakazi katika sekta nyingine kupigania nyongeza za mishahara.
Huku zikiwa zimesalia siku 145 Uchaguzi Mkuu kufanyika Rais Uhuru Kenyatta amechukua fursa ya hotuba hiyo kujipigia upatu ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.
Kinyume na hotuba ya mwaka uliopita, hotua ya mwaka huu haikukatizwa na wabunge wa upinzani kama walivyokuwa wameapa kufanya ikiwa Rais hangeomba msamaha wananchi kwa matamshi yake ya matusi katika siku za hivi karibuni.
Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza matayarisho ya uchaguzi ujao.
Tayari kesi kadhaa ziko mahakamani kupinga utaratibu wa tume ya uchaguzi nchini tume ya huru ya uchaguzi nchini humo IEBC.
Rais Uhuru Kenyatta amekumbana na upinzani mkali katika kipindi chake cha kwanza kinachomalizika mwezi wa nane mwaka huu akilaumiwa kwa kukithiri kwa ufisadi, kuzorota kwa usalama na kupanda kwa gharama ya maisha.
Baada ya kulihutubia taifa kiongozi huyo alifungua rasmi jengo la Baraza la Senate na kusema ufunguzi wa ukumbi wa Senete ni ishara ya kuimarika kwa mamlaka ya ugatuzi.
Raila Odinga atamshinda Kenyatta?
Raila Odinga ndiye amekuwa akionekana tishio kwa Uhuru Kenyata na vyama tawala kwenye chaguzi mbalimbali ingawa bado hajawahi kufanikiwa kupenya na kuingia Ikulu.
Odinga si mtu wa kukata tamaa amedumu kwenye siasa za Kenya kwa muda mrefu na huwa haoni woga kuikosoa serikali kila inapobidi.
Awali ilielezwa kuwa katika chama cha CORD, kulikuwa na mvutano kuhusu nani anastahili kupeperusha bendera ya muungano huo, dhidi ya muungano wa Jubilee.
Hata hivyo, gazeti moja hapa nchini liliwahi kumnukuu mwenyewe, akisema kwamba yuko tayari kumuunga mkono yeyote atakayesimamia kiti cha ugombea urais katika chama cha CORD ili kumshinda Kenyatta.
Raila Odinga alikuwa katika ziara eneo la pwani katika mpango wa kuuza chama cha ODM ili kuimarisha uungwaji mkono wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2017.
Ingawa Uhuru amekuwa akijitahidi, lakini serikali yake imekumbwa na changamoto nyingi sana, mojawapo ikiwa ni ufisadi, ugaidi na mengine mengi. Wakenya wengi wanamtizama kwa jicho la karibu sana kulingana na namna anavyojaribu kukabiliana na changamoto hizo.
Baadhi ya viongozi wa fedha wa mataifa mbalimbali ulimwenguni waliwahi kumpongeza Rais Kenyatta kwa mtazamo na uongozi bora ambao wanasema ni muhimu katika ukuaji wa Bara la Afrika.
Kiongozi wa Benki ya Dunia na African Development Bank (AFDB) alisema sera za Kenya zilizoanzishwa na Rais Kenyatta zimeweka mazingira mazuri ambayo yamechangia uwekezaji na biashara kati ya mataifa ya Afrika.
Vyama vya upinzani vimejipangaje?
Vyama vya upinzani vimeshazindua muungano unaojulikana kwa kifupi kama National Super Alliance "NASA" kwa ajili ya kukabiliana na muungano unaotawala wa Jubilee vimesisitiza kudumisha umoja wao ili kuiondoa madarakani serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kupitia uchaguzi mkuu ujao.
Kuweko mshikamano wa kitaifa, kupambana kwa dhati na ufisadi, umasikini na ukosefu wa usalama ndizo nguzo kuu za muungano huo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Pilikapilika na hekaheka za kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini Kenya zinashuhudiwa katika hali ambayo, kwa muda sasa anga ya kisiasa ya nchi hiyo imetawaliwa na wingu la vuta ni kuvute baina ya wanasiasa wa upinzani na wenzao walioko serikali.
Inaonekana kuwa, licha ya kuweko juhudi za serikali pamoja na mazungumzo ya wawakilishi wa vyama vya upinzani, bado kuna hitilafu nyingi ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi.
Raila Odinga mwanasiasa mtajika na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya ametahadharisha kuhusiana na hatua yoyote ile ya udanganyifu katika zoezi la uchaguzi.
Odinga sanjari na kuituhumu serikali ya Jubilee kwamba, inafanya mikakati ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi ujao, amewataka wafuasi wake wafanye maandamano dhidi ya serikali ya Rais Kenyatta.
Wasiwasi wa wapinzani wa kufanyika udanganyifu katika uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya unatokana na mabadiliko ya sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni katika Bunge la nchi hiyo na Wabunge wa Jubilee baada ya Wabunge wa upinzani kususia zoezi hilo.
Kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria hizo ni kuwa, endapo mitambo ya kuhesabia kura itakwama na kutofanya kazi, basi zoezi hilo litaendelea kwa kuhesabu kura kwa mfumo wa mkono.
Wapinzani nchini Kenya wanaamini kuwa, hatua hiyo inaongeza uwezekano wa kufanyika udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi huo.
Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuongezeka kwa mivutano ya kisiasa nchini Kenya kunatishia uwezekano wa kutokea machafuko mengine kama yale yalitokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Katika uchaguzi huo Raila Odinga alishindwa na Mwai Kibaki. Mgogoro na machafuko ya kikabila uliibuka baada ya Raila Odinga kukataa matokeo ya uchaguzi huo.
Machafuko hayo yalisababisha watu zaidi ya 1,500 kuuawa na wengine zaidi ya laki tatu kubaki bila makazi, huku kukishuhudiwa hasara kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, machafuko ya uchaguzi nchini Kenya yaliyotokea kati ya Desemba 2008 na Februari 2008, ni jambo ambalo linapaswa kuwafanya wanasiasa wa nchi hiyo kuwa na moyo wa subira zaidi ili kuzuia kuitumbukiza tena nchi hiyo katika dimbwi lingine la vurugu na machafuko.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika hali ya hivi sasa Kenya inakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi kufuatia kupungua pato la taifa linalotokana na sekta ya utalii ambayo inahesabiwa kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa nchi hiyo.
