Zitto: Rais Magufuli ametia hasara nchi ya Ths trilioni 1.8


Kupitia ukurasa wake wa FaceBook kiongozi huyo ameandika hivi..
Jana nilipokuwa natoa mada kuhusu miaka 50 ya Azimio la Arusha niliongelea pia suala la umakini wa viongozi katika kauli zao. Kwamba Kiongozi lazima ujue unatoa kauli gani wakati gani. Niliwaeleza wanachama na wageni wengine katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa Amri ya kiholela aliyoitoa Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa Mchanga wa Dhahabu imepelekea nchi yetu kupoteza USD 880m Kama kodi ya ongezeko la Mtaji kutokana na mauzo ya Acacia Mining.

Hivi sasa nchini kwetu kuna sheria ya kutoza 20% ya thamani ya mauzo iwapo kampuni zinauziana hisa. Tozo inayotozwa inaitwa Capital Gains Tax. Kodi hii mpya ilitungwa mwaka 2012 ili kukabili wawekezaji waliokuwa wanauziana makampuni juu Kwa juu bila Tanzania kupata lolote. Tanzania imeshafaidika na kodi hiyo Kwa mauzo mbali mbali ambayo yamekwisha fanyika kwenye sekta mbalimbali.

Wakati Rais anatoa AMRI kuhusu Mchanga wa madini kusafirishwa kwenye nje ya nchi kulikuwa na mazungumzo yanaendelea kati ya Kampuni ya Acacia mining ( yenye Assets zinazozalisha nchini Tanzania tu kwa sasa - Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyengine ya nchini Canada kuhusu Acacia kununuliwa Kwa USD 4.4bn. Mara baada ya amri hiyo mazungumzo yalivunjika na hivyo mauzo kutofanyika. 

Iwapo Rais angechelewa kutoa kauli yake Kwa wiki moja tu mazungumzo yale yangepelekea mkataba wa mauzo kusainiwa na hivyo Serikali ingepata 20% ya thamani ya Mauzo Kama kodi ya Ongezeko la Mtaji ( capital gains tax ). Hivyo kauli ya Rais imesababisha hasara Kwa nchi yenye thamani ya USD 880m sawa sawa na shilingi 1.8 trilioni.

Tafiti zinaonyesha kuwa gharama ya kujenga ' refinery ' ya kuchenjua dhahabu hapa nchini ni USD 800m. Hivyo mapato ambayo yangepatikana kutokana na kodi ya mauzo ya Acacia yangewezesha nchi kujenga refinery na kufikia lengo la Rais la kuwa na uchenjuaji wa mchanga ule hapa hapa nchini. Rais angetulia angeweza kuua ndege wawili Kwa jiwe moja, 1) kiwanda cha kuchenjua kingejengwa nchini na 2) mchanga usingesafirishwa tena kwenda China na Japan.

Hata hivyo Tanzania haina mchanga wa kutosha wa kushibisha hiyo refinery Kwa mujibu wa teknolojia ya sasa ( soma maelezo yangu hapa chini Kwa Mhariri wa RaiaMwema). Hivyo Rais angeweza kutumia mapato hayo Kwa matumizi mengine ya Maendeleo. Kwa mfano Bunge lilitenga kama USD 430m hivi kujenga Reli ya kisasa na tayari Serikali imeshaingia mkataba na kampuni kutoka Uturuki kujenga Reli hiyo kipande cha Dar es salaam mpaka Morogoro. Lakini gharama ya kipande hicho ni USD 1.2bn. Kwahiyo Rais angeweza kutumia mapato haya ya mauzo ya Acacia kuongezea kwenye kipande hiki na hivyo kuepuka kukopa kuziba nakisi ya USD 800m iliyopo Sasa na Bunge kwenye Bajeti ya 2017/18 lingetenga fedha za kuanzia Morogoro kwenda Dodoma.

Kama Mipango ya Reli ipo sawa, Rais angeweza kutumia fedha za capital gains tax kutoka Acacia kujenga vyuo vya VETA kila Wilaya na kila Kambi ya JKT na chenji ingebaki. Tanzania inahitaji tshs 750 bilioni kujenga vyuo vya VETA kila Halmashauri ya Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji nchini.

Rais angejifunza kujizuia kutoa matamko barabarani angeisaidia Sana nchi na kujisaidia yeye mwenyewe kutimiza ndoto zake kwa nchi anayoongoza. Mimi binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue dhahabu hapa hapa nchini badala ya kupeleka mchanga Japan na China. Lakini ni muhimu maamuzi hayo yawe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko holela ambayo madhara yake Kwa nchi ni makubwa mno.

Zitto Kabwe, Mb 
Arusha 
26/3/2017