Mbunge akosoa marufuku viroba

MBUNGE wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM) amesema ni vyema serikali ingezuia uzalishaji wa viroba badala ya kuwazuia wafanyabiashara kuuza pombe hiyo na kuwasababishia hasara ya mabilioni.

Aidha, Shabiby alishauri serikali itumie namna bora ya kuzuia viroba kwa kuwa utaratibu uliotumika umesababisha madhara.

Akichangia juzi hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/18, Shabiby alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17 kodi iliwekwa kwenye pombe hizo na ilipitishwa kihalali.

“Utaratibu wa kuzuia vitu hivi uanze viwandani ili wafanyabiashara ambao tayari walikuwa na stock (akiba) zao wamalizie kuuza,” alisema.

Alitaka utaratibu uliotumika wa kuwazuia wafanyabiashara kuuza usitumike tena kwa kuwa umewasababishia hasara kubwa.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wa pombe ya viroba walilazimika kufunga biashara kutokana na kukabiliwa na madeni makubwa waliyokopa katika taasisi za fedha.

Hata hivyo, Shabiby alipongeza hatua ya serikali ya kupiga marufuku pombe hiyo na kwamba hivi sasa watu waliokuwa wanatumia wameanza kunenepa kutokana na kuacha kutumia kinywaji hicho.

“Sio kama mimi naunga mkono matumizi ama biashara hii ya viroba, lakini anapinga utaratibu uliotumika kuzuia biashara hii kwani ulikuwa wa ghafla mno na kusababisha madhara kwa wafanyabiashara.”

Miezi miwili iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kufikishwa mahakamani mtu yeyote atakayekamatwa na pombe ya viroba iliyofungashwa kwenye plastiki, kuanzia Machi mosi.

Waziri Mkuu alitoa taarifa hiyo wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika ziara yake mkoani Manyara.

“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika," alisema.

“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona, (na) hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo.

"Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”

Amesema agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
Mpya zaidi Nzee zaidi