DONALD NGOMA.
WAKATI wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Yanga wakiwa tayari kuvaana na wapinzani wao Mouloudia Club Alger maarufu kama MC Alger, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha George Lwandamina limesema ushindi ni muhimu leo.
Yanga inawakaribisha klabu hiyo ya Algeria kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo unaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe jana, Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema kikosi cha timu hiyo kipo kamili kuwakabili waarabu hao.
"Ni mchezo ambao umekuja huku tukiwa na ahueni ya majeruhi..., kama mnakumbuka tulikuwa na wachezaji wetu nyota ambao wlaikosa michezo kadhaa kwa kuwa walikuwa wanauguza majeraha, lakini wengi wao wamerejea uwanjani na watakuwepo mchezo wa kesho," alisema Mwambusi.
Alisema, watacheza soka la kushambalia na kujaribu kusaka bao la mapema ili kuwachanganya wapinzani wao hao.
"Tunafahamu kuwa tunahitaji kupata ushindi mzuri ili tusiwe na kazi kubwa ugenini kwenye mchezo wa marudiano..., tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Mwambusi.
Mwambusi, alisema kwenye mazoezi ya mwisho ya jana asubuhi wachezaji wa timu hiyo walionyesha morali ya juu kuelekea kwenye mchezo wa leo.
"Wachezaji wa Yanga wako na morali ya hali juu na kikubwa tunawaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hii kwa sababu ni klabu pekee iliyobaki ikiiwakilisha nchi,”alisema Mwambusi.
Yanga leo itakuwa na nyota wake, Donald Ngoma, Amis Tambwe na Thaban Kamusoko ambao walikosa mchezo uliopita wa ligi Kuu dhidi Azam ambao Yanga walishinda kwa bao 1-0.
Mchezo huo wa leo utachezeshwa na mwamuzi Louis Hakizimana akisaidiwa na waamuzi wa pembeni Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka wote kutoka Rwanda.
Yanga itarudiana na klabu hiyo Aprili 14 nchini Algeria kabla ya kufahamu hatma yao ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.