Yanga bado tupo imara: MKWASA

KATIBU MKUU WA TIMU HIYO CHARLES MKWASA.

SIKU chache baada ya kukiri kushindwana na kiungo wake Haruna Niyonzima, Katibu Mkuu wa timu hiyo Charles Mkwasa, amesema timu hiyo bado ipo imara na wapo kwenye mkakati wa kusajili kiungo mwingine.

Mkwasa, alisema walikuwa na nia ya kumbakisha kiungo huyo lakini kwa sasa wanaangalia mambo mengine ikiwa pamoja na kutafuta kiungo mwingine kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao.

“Kwa sasa tunaendelea na mikakati mingine, yapo mapendekezo ya kocha ambayo tunayafanyia kazi.., mmoja wa wachezaji tunayetaka kumsajili ni wa nafasi ya kiungo,” alisema Mkwasa.

Aidha, alisema kuwa suala la usajili la klabu hiyo linaendelea na wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji kwa ajili ya kuwasajili.

“Kuna mapendekezo ya kocha wetu kwenye ripoti yake na sisi kama viongozi ndio tunayoifanyia kazi, wana Yanga wasiwe na wasiwasi timu itakuwa imara msimu ujao,” alisema Mkwasa.

Yanga inatajwa kuwa tayari imemalizana na mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib huku ikitangaza kuachana na Niyonzima baada ya kushindwana kwenye dau la usajili.

Niyonzima anajiandaa kutua kwa mahasimu wao Simba kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, nahodha huyo wa Rwanda atasaini mkataba wa miaka miwili.