MADIWANI Halmashauri ya Chalinze, wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Kamati ya fedha wameiagiza idara ya fedha kumchunguza Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Matuli kwa tuhuma za kukusanya mapato akitumia risiti ya kitabu chenye nembo ya Sungura badala ya nyaraka zinazotambuliwa.
Mwandishi wa habari alimshuhudia Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Zikatimu akitoa agizo kwa maofisa Idara za fedha, biashara na mipangomiji akisema kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa serikali kutumia vitabu 11 vyenye nembo ya Sungura badala ya vinavyotambuliwa na halmashauri ni kitendo cha kuwakosesha mapato wananchi wake na hivyo ametaka wakaguzi waende mara moja kuchunguza.
Akiambatana na madiwani Mhandisi Juma Mgweno (Mkange), Hussein Juma Hading'oka (Kimange), Hassani Mwinyikondo (Msoga) Mwanakesi Madega Tarafa ya Bwilingu na wataalamu, ziara hiyo inayotembelea vijiji vinavyounda Kata mbalimbali ilianzia Julai 22 ambapo Zikatimu alisema kuwa bado kuna baadhi ya viongozi na watu waliopewa jukumu la kusimamia mapato wanakwamisha juhudi hizo.
"Tangu Julai 22 tukiwa katika vijiji tumeshudia ukwepaji wa mapato unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanaosimamia zoezi hilo, pale Dihozile kuna unafuu, tulikwenda mara ya kwanza walisema kwa siku gari moja, leo tumeambiwa gari 15, Msoga Mtendaji wa Kijiji hakusanyi kabisa, Matuli Mwenyekiti tumemkuta na vitabu aina ya Sungura 11, wakaguzi wa ndani waende mara moja kuchunguza," alisema Zikatimu.
Kwa upande wake Mwinyikondo akiwa katika Kijiji cha Vigwaza alisikitishwa na hali aliyoikuta ambapo mkusanyaji ushuru wa halmasbauri hakuwa katika eneo lake kwa siku nne huku anayekusanyia kijiji akiendelea na kazi ya kuchukua sh. 5,000 kwa kila gari zinazokwenda kijijini wakati halmashauri haipati kitu.
Hading'oka alielesea masikitiko yake kufuatia kiwepo kwa watu wanaotarajiwa kuitumika halmashauri lakini kinyume chake wanashindwa kutekeleza majukumu yao huku akitaka wasiowajibika watumbuliwe kwenye nafasi zao ili wapatiwe wenye uwezo na uchungu wa halmashauri.
Mhandisi Mgweno alisema kuwa kutokana na halmashauri hiyo kupoteza mapato mengi wakati vijiji vinakusanya, ameomba kuwepo kwa hesabu elekezi ya kuyoza ushuru ambapo kwa magari yenye tani kuanzia 3 mpaka 6 zilipie sh. 6,000 zinazozidi uzito huo zitozwe zaidi ya kiasi hicho.
