Kiongozi wa waandalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) Thabo Mbeki amesema shughuli ya upigaji kura nchini Kenya ilikuwa ya uwazi na waangalizi hao waliridhishwa na shughuli hiyo.
Hata hivyo amesema kulikuwa na changamoto kadha, mfano ingawa karatasi zilikuwa za rangi tofauti pamoja na masanduku, kulikuwa na rangi mbili ambazo zilikuwa zinakaribiana sana.
Hata hivyo, amesema maafisa wa uchaguzi waliwasaidia wapigaji kura kutofautisha rangi hizo.
Bw Mbeki ameipongeza pia serikali na tume kwa kuhakikisha wafungwa walipiga kura.
"Tunafahamu kwamba IEBC bado inahesabu na kukagua matokeo. Shughuli ya uchaguzi bado inaendelea hivyo bado ni mapema hivyo. Hata hivyo, waangalizi wa AU wanafurahi kwamba uchaguzi ulikuwa wa amani, siku ya uchaguzi watu walifika kwa wingi, na waliruhusiwa kuopiga kura kwa kufuata taratibu za uchaguzi Kenya na zinazokubaliwa na AU," amesema.
Tunaweza kusema kwamba shughuli tulizohesabu, upigaji kura na upeperushaji wa matokeo, vilitimiza viwango vya ubora vya Kenya na AU.
Amesema wamepokea malalamiko kuhusu upeperushaji wa matokeo. Ametoa wito kwa wadau kutumia mifumo wa kisheria iliyopo.
Bw Mbeki amesema maafisa wa Nasa walikutana na waangalizi wa AU na kuwapa ripoti kuhusu madai ya udukuzi wa mitambo ya IEBC.
Amesema waliulizwa walipata vipi nyaraka walizokuwa nazo za madai ya udukuzi. Walisema walikuwa wamepewa 'ufunguo' fulani na IEBC wa kuweza kuingia kwenye sava.
Hata hivyo, tuliwaambia kwamba kwa kufuata fomu 34A itawezekana kwa kila mtu kubaini matokeo halisi.
Upinzani hata hivyo ulitilia shaka uhalisi wa fomu hizo na kusema katika baadhi ya vituo vya kupigia kura hawakuwa na maajenti na katika baadhi, maajenti wao walizuiwa kuingia.
Aidha, upinzani ulisema huenda fomu 34A katika baadhi ya vituo zilifanyiwa mabadiliko.
