Fainali Kombe la Ligi leo ni Wenger vs Guardiola

Kwa mara ya kwanza Arsenal na Manchester City wanakutana katika fainali kubwa hii leo, Wenger anatafuta kombe lake la kwanza la ligi huku  Pep Gurdiola akitafuta kombe la kwanza nchini Uingereza.

Timu hizi mbili mwaka 2014 zilikutana katika fainali ya Ngao ya Hisani ambapo Arsenal waliichapa Man City bao 3-0 lakini pia wakakutana katika mchezo wa nusu fainali ya FA ambapo Gunners waliichapa tena City bao 2-1.

Mara nyingi timu hizi mbili zimekutana katika mechi za EPL na rekodi zinaonesha katika mechi 5 zilizopita kati ya Arsenal na City katika EPL, City wamepoteza mara moja tu lakini wakashinda mara 2 na pia wakapata suluhu mara 2.

Katika kikombe hiki cha ligi ukiacha mara mbili ambazo City wameifunga Arsenal (2009/2010 na 2011/2012) ,lakini kabla ya hapo Manchester City hawajawahi kuwafunga Arsenal katika kikombe cha ligi kuanzia msimu wa 1977/1978 hadi msimu wa 2004/2005.

Kwa Arsenal hii ni fainali yao ya 8 na ndio klabu inaongoza kwa kupoteza fainali nyingi kwani katika fainali hizo wamepoteza fainali 5 za mshindano hayo na wakafanikiwa kushinda fainali mbili (1987 na 1993).

Hii leo itakuwa mara ya sita kwa Manchester City kucheza fainali ya kombe la ligi na itakuwa mara ya 3 katika misimu mitano iliyopita, katika fainali hizo Man City wameshinda fainali 5 na mara pekee waliyoshindwa ni msimu wa 1974.