Korea Kaskazini yataka suluhu na Marekani

Korea Kaskazini ina nia ya kufanya mazungumzo na Marekani, kwa mujibu wa Korea Kusini, tangazo hilo limekuja baada ya Jenerali Kim Yong-Chol kukutana na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, kabla ya sherehe za kufungwa kwa mashindano ya olimpiki wa msimu wa baridi.

Ivanka ambaye ni binti wa Rais wa Marekani Donald Trump pia alihudhuria sherehe hizo, lakini maafisa wa Marekani wamekana kufanya mkutano na ujumbe kutoka Korea Kaskazini.

Marekani inasema Korea Kaskazini ilijiondoa kwenye mkutano na Makamu wa Rais Mike Pence wakati wa sherehe za ufunguzi.

Eneo la rasi ya Korea limegawanyika tangu vita vya mwaka 1950 hadi 1953 na pande hizi mbili hazijawai weka sahihi mkataba wa amani.

Uhusiano baina ya Korea Kaskazini na Kusini umeonekama kama njama ya Korea kuvuruga ukaribu kati ya Korea Kusini na Marekani.

Hata hivyo wataalamu wanaonya kuwa mazungumzo yanayofanyika sasa hayamalizi kikomo wala misukosuko ya kieneo hasa kufuatia majaribio ya nyuklia na ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini.

Siku ya Ijumaa Marekani ilitangaza awamu mpya ya vikwazo dhidi ya korea Kaskazini.