Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi mbalimbali ambayo yatadhoofisha afya yake. Hivyo basi ni muhimu kwa mtu huyo au mtayarishaji wa chakula kuzingatia yafuatayo ili kufanya chakula na maji viwe safi na salama kwa mtumiaji:
- Vyombo vinavyotumika kutayarishia na kupakulia chakula viwe safi. Vyombo vioshwe vizuri kwa sabuni kabla ya kutumia. Majivu yatumike pale ambapo hakuna sabuni.
- Sehemu zote za kutayarishia chakula ziwe safi.
- Funika vyakula na maji na hifadhi katika hali ya usafi kuzuia wadudu hasa inzi.
- Hakikisha chakula kimepikwa na kuiva vyema, na pia kiliwe kingali cha moto.
- Osha matunda na mboga-mboga kwa maji ya kutosha, ikiwezekana yaliyochemshwa.
- Sehemu zenye michubuko katika mboga na matunda zikatwe na kutupwa.
- Epuka kutumia vyakula vilivyosindikw a ambavyo muda wake wa kutumia umekwisha.
- Epuka nafaka au vyakula vilivyoota ukungu.
- Hakikisha kuwa nyama, samaki na mayai vinapikwa na kuiva vizuri ili kuepuka maambukizo ya magonjwa (vyakula hivi kamwe visiliwe vikiwa vibichi). Vyombo na vifaa vinavyo tumika kutayarisha nyama mbichi, samaki wabichi na mayai mabichi vioshwe vizuri kwa sabuni kabla ya kuvitumia kwa matumizi mengine. Majivu yatumike pale ambapo hakuna sabuni.
- Vyakula vilivyokaa zaidi ya saa mbili baada ya kupikwa au viporo, ikibidi kuliwa vipashwe moto vizuri kabla ya kuliwa hata kama bado vina uvuguvugu.
- Epuka mgusano wa vyakula vibichi na vile vilivyopikwa, hasa nyama mbichi, samaki wabichi na mayai mabichi. Hakikisha maji ni safi, chemsha maji na acha yaendelee kuchemka kwa muda wa dakika 5 hadi 10.
- Tunza maji katika chombo safi chenye mfuniko. Iwapo unahitaji kutumia barafu hakikisha maji yaliyotumika kutengenezea barafu yamechemshwa.
Tags:
Afya
