Waziri Jenista ataka vijana kuchangamkia fursa

Serikali imewataka wafanyabiashara nchini kuanza kujiandaa kuzitumia fursa zilizopo katika ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Kabaale Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani, Tanga Tanzania kwa vile asilimia 80 ya bomba la mradi litapita nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama ametoa changamoto hiyo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua kongamano la siku moja la kujadili ushiriki wa watanzania katika mradi huo na kuwataka wafanyabiashara nchini wajiandae kushiriki katika mradi huo kwa kuwa asilimia kubwa ya bomba hilo litapita nchini.

Waziri Mhagama amesema mradi huo mkubwa unatarajiwa kufanyika hapa nchini kwa thamani ya Dola za kimarekani billioni 3.5, na kuwataka watanzania kujiandaa kutumia fursa zitakazo jitokeza katika mradi huu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa amesema lengo la kongamano hilo lilikuwa ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka sekta ya Umma na binafsi ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu mradi huu huo na fursa zake ili waweze kujitayarisha mapema huku Mkurugenzi wa Gesi Asilia kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA), Mhandisi Charles Omujuni na Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Louis Accaro wakieleza namna walivyojipanga kutekeleza majukumu yao