Na Thabit Madai, Zanzibar
Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi amesema Tasisi zinazosimamia uingizwaji na udhibiti wa dawa za kulevyya nchini zikijipanga kikamilifu zinaweza kuondoa na kupunguza usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
Ameitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na kamati ya tume ya kitaifa ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya Zanzibar mara baada ya kukamilisha ziara fupi ya kukagua mazingira ya kazi ya wafanya kazi wa tume hiyo,
Balozi seif amesema Zanzibar haina mahali pengine panapotumiwa kwa uingizaji na utoaji wa Dawa za Kulevya isipokuwa Bandarini na Viwanja vya Ndege maeneo ambayo kama mikakati ya kizalendo itatumiwa na wasimamizi wake uwepo wa Dawa za kulevya itakuwa historia katika Taifa hili.
Amesema licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali Kuu kwa kushirikiana na Taasisi za Kitaifa na Kimataifa za kuendesha mapambano dhidi ya Uingizwaji na usambazaji wa Dawa la kulevya lakini bado wapo baadhi ya Watendaji wanashindwa kuwa waadilifu katika mapambano hayo.
Balozi Seif ameeleza kwamba upo ushahidi unaoonesha kwamba baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma kama Polisi na Mahakama sio waaminifu kwa kutoa mwanya kwa Wafanyabiashara wa Dawa za Kulevya kukwepa Kesi zinazowakabili na hatimae kuendelea kufanya biashara hiyo haramu.
Alitanabahisha kwamba kila sekta ikiamua kutimiza wajibu wake iliyopangiwa na Taifa , wimbi la Dawa za kulevya Nchini linaloikumba Jamii hasa kundi kubwa la Vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa linaweza kuondoka.
Aidha Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji pamoja na kuwashukuru Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kutekeleza majukumu yao ya kazi ya kilaSiku katika mazingira magumu na kuahidi kuwajenga ofisi mpya.
“Kazi hii nitamuachia Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wao kukaa pamoja na Uongozi wenu kufikiria eneo litakalofaa ili tukujengeeni Ofisi inayolingana na kazi zenu nzito za kila siku zinazohitaji utulivu ”.Alisema Balozi Seif.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo Bi. Kheriyangu Mgeni Khamis amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo wimbi la uingizwaji wa Dawa za Kulevya linalotokana na uwepo wa baadhi ya wasimamizi wasiokuwa waaminifu na kupelekea waendesha Biashara hiyo kupata mwanya wa kuendelea na mchezo huo mchafu.
Amesema changamoto nyengine ni uchakavu na ufinyu wa Ofisi ya Tume unaopelekea kuwa na watendaji kidogo licha ya Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma kutoa baraka ya nyongeza ya Wafanyakazi wa Tume hiyo.
Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar inasimamiwa na Watendaji 35 wenye uzoefu mkubwa na sifa tofauti za Kielimu katika masuala ya Afya, Utawala, ushauri nasaha pamoja na Ukaguzi wa Dawa za Kulevya.
