Wema aingilia kati ugomvi wa Zamaradi na Mobeto

 DAR ES SALAAM: Wakati bifu baina ya mtangazaji wa runinga, Zamaradi Mketema na mwanamitindo Hamisa Mobeto juu ya gauni la kushona likishika kasi, mrembo Wema Isaac Sepetu ameibuka na kununua ugomvi huo. Ishu nzima ilianzia Jumanne ya wiki hii ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zamaradi aliandika waraka mrefu wa kurasa tatu ukieleza namna
alivyosikitishwa na Mobeto kwa sababu ya gauni alilovaa katika arobaini ya mtoto wake aitwaye King Salah iliyofanyika mwishoni mwa Julai, mwaka huu nyumbani kwake maeneo ya Bunju B jijini Dar.

Katika waraka huo, Zamaradi alionesha kusikitishwa na maneno yanayosambaa mitandaoni kuwa alipewa mshono na Mobeto kwa lengo la kushonewa, lakini akauchukua na kwenda kuushona kwa mtu mwingine huku akimwaga chati zote za WhatsApp walizokuwa wakitumiana.
 Hata hivyo, kwa upande wa Mobeto naye aliibuka na kupinga vikali waraka huo. Wakati hayo yakiendelea, Wema kupitia ukurasa wake alinunua ugomvi kwa kuandika; Tuendelee ama tusiendelee’ ambapo swahiba wake wa karibu ambaye ni mbunifu wa mavazi, Martin Kadinda aliingilia kati kwenye komenti na kuandika; ‘Tusiendelee’.

Muda mfupi mara baada ya Wema kusema hayo, aliambulia maneno machafu kutoka kwa mashabiki tofauti wakimlaumu; “Ni bora ungekaa kimya kuliko kuingilia mambo yasiyokuhusu*** wee,” alikomenti shabiki mmoja huku wengine wakishadadia.

Meneja wa Wema, Neema Ndepanya naye hakukaa kimya, aliingilia kati na kumkingia kifua Wema kwa kuandika waraka wake. “Kiki za kuchafuana zilishapitwa na wakati, hakuna kitu kibaya duniani kama kuwa mnafiki, yaani nachukia mtu anajifanya kila wakati anaonewa yeye tu,” aliandika.
Baada ya kuyaona hayo yakiendelea mitandaoni, Ijumaa lilianza kwa kumsaka mnunua ugomvi, Wema ambaye simu yake iliita bila kupokelewa, likampigia simu Neema na alipopatikana alisema hajamkingia kifua Wema na hayupo upande wa mtu yeyote.

“Sasa unaniuliza mimi kwani ndiyo Zamaradi, Wema au Hamisa si uwapigie wahusika mimi ni mpenzi mtazamaji tu kama wewe sihusiki na chochote na wala sipo upande wa yeyote kati yao. Kama watu wametafsiri vingine ni shida yao mimi simo kabisa si unajua kila mtu anaandika kitu anachojisikia eeh basi nimejisikia tu kuandika mtu akisoma vizuri ataielewa, lakini ukikurupukia kuisoma lazima ulete maana nyingine,” alisema Neema.