Hizi ndizo rekodi 5 zinazomtesa Messi


Messi

LIONEL Messi ni mwenye akili sana dimbani hatua ya kumfanya kila mtu aamini kuwa hakuna rekodi muhimu aliyobakisha kuiweka katika soka.

Nyota huyo wa Barcelona mwaka huu alikosekana katika kinyang'anyiro cha Mchezaji Bora wa Mwaka wa FIFA, lakini bado anaendelea kuelezwa na wengi kama mchezaji mkubwa dimbani.

Nahodha huyu wa Argentina, ana tuzo nyingi za soka duniani mikononi mwake na tuzo tano za Ballon d’Or alizo nazo ni chache kuweza kuthibitisha ubora wake. Mapema wiki iliyopita kwa mara nyingine Messi aliiwezesha Barcelona kushinda 4-2 dhidi ya Tottenham kwenye mechi ya hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Messi, 31, alicheka na nyavu mara mbili katika ushindi huo na angeweza kutupia hata hat-trick kama isingekuwa ubora wa kipa wa Spurs, Hugo Lloris. Na mabao hayo yanamfanya Messi kucheka na nyavu mara tano kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa katika mechi mbili walizocheza hadi sasa msimu huu.

Muargentina huyo pia ana makombe manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na inaelezwa itachukua muda mrefu kabla ya dunia kushuhudia tena kipaji kingine kama cha Messi.

Hata hivyo, licha ya ubora wake dimbani, bado kuna idadi kubwa ya rekodi ambazo Messi hajaweza kuzivunja wakati linapokuja suala la soka barani Ulaya. Anaweza kuzivunja na kutengeneza nyingine, lakini kuna rekodi zaidi ambazo hajakaribia kuzivunja. Na hapa ni rekodi tano ambazo nahodha huyo wa Barca bado hajazivunja...

5. Kucheza mechi nyingi michuano Uefa

Rekodi nyingine katika michuano ya Ulaya ambayo Messi bado hajaifikia rekodi hiyo ya kucheza mechi nyingi. Nyota huyo wa Barcelona alicheza mechi yake ya kwanza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2004-05 akiwa kama kinda, lakini aliendelea haraka na kupata nafasi ya mara kwa mara kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Catalunya.

Kwa kuanza mechi ya Jumanne iliyopita dhidi ya Tottenham, Messi sasa ameshuka dimbani mara 128 kwenye michuano hiyo ya Ulaya. Kwa kuzingatia ndiyo kwanza ana miaka 31 tu, anaweza kushuka dimbani zaidi kwenye michuano hiyo kwa miaka ijayo.

Messi ana miaka michache ya kuendelea kuwamo dimbani kwa kiwango cha juu, lakini mchezaji anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi ya michuano hiyo ni kipa wa zamani wa Real Madrid, Iker Casillas. Kipa huyo wa Porto kwa sasa, alicheza kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema miaka ya 1990, ikiwa ni miongo miwili iliyopita.

Hadi sasa Casillas ameshashuka dimbani mara 179 kwenye michuano hiyo, idadi ambayo haijafikiwa na mchezaji yeyote yule na si Messi pekee.

4. Mabao Mengi Fainali

UEFA

Kadhalika, Messi licha ya kucheza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne, idadi yake ya mabao haivutii.

Messi amecheka na nyavu mara mbili tu kwenye mechi za fainali na yote alifunga walipokutana na Manchester United fainali mwaka 2009 na  2011.

Straika huyo wa Barca alishindwa kufunga katika fainali mbili na hivyo kufanya rekodi hiyo kuendelea kushikiliwa na wakongwe wawili wa Real Madrid, Ferenc Puskas na Alfredo Di Stefano ambao kila mmoja amecheka na nyavu mara saba katika fainali, lakini pia rekodi hiyo bado haijafikiwa na mchezaji mwingine yeyote na si Messi tu.

3. Mabao mengi

msimu mmoja UEFA

Messi amebandikwa mabao kila sehemu ya mwili wake. Licha ya kutokuwa straika, nyota huyu wa Barcelona anaweza kutoa upinzani kwa mshambuliaji yeyote mchezoni kwa sasa. Muargentina huyu ameshinda tuzo nyingi za ukinara wa ufungaji, zote Hispania na Ulaya, lakini bado hajafurukuta katika kuwa kinara wa ufungaji kwenye msimu mmoja wa michuano ya Ulaya.

Kufuatia Jumatano iliyopita kuibuka shujaa kwa kuibanjua Tottenham mara mbili, Messi kwa sasa ana mabao 105 katika michuano hiyo ya Ulaya. Hata hivyo, wakati linapokuja suala la mabao mengi kwa msimu mmoja, nahodha huyo wa Argentina hamkuti Cristiano Ronaldo na Radamel Falcao.

Wote Ronaldo na Falcao wanashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kwa msimu mmoja kwenye michuano hiyo kila mmoja akicheka na nyavu mara 17. Falcao aliweka rekodi hiyo msimu wa 2010-11 wa Europa League, wakati  Ronaldo alitupia idadi hiyo msimu wa 2013-14 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hadi sasa Messi idadi kubwa ya utupiaji kwa msimu mmoja wa michuano hiyo ya Ulaya ni mabao 14, ambayo alifunga msimu wa 2011-12.

2. Bao la mapema zaidi UEFA

Messi amevunja na kuweka rekodi nyingi katika wasifu wake kisoka, lakini rekodi ya bao la mapema zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya siyo sehemu ya uwezo wake. Hii ni moja kati ya rekodi chache ambazo Muargentina huyo hajaivunja.

Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or, ameipoteza rekodi hiyo kutoka kwa nyota wa kimataifa wa zamani wa Uholanzi, Roy Makaay, ambaye alifunga baada ya sekundi 10.12 tu tangu mpira kuanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Bayern Munich na Real Madrid mwaka 2007 ambao hadi sasa linabaki kuwa bao la mapema zaidi katika michuano hiyo ya UEFA.

1. Hat-trick ya mapema zaidi Uefa

Hadi sasa Messi ameshafunga mabao 105 Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kati ya idadi hiyo kuna hat-trick moja, mbili na hata kuna wakati alitupia mara tano katika mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Muargentina huyo ana jumla ya hat-trick sita kwenye michuano hiyo– ambazo zinamfanya kuwa mchezaji mwenye hat-trick nyingi, lakini bado hazimfanyi kuwa kinara pindi linapokuja suala ya hat-trick ya mapema zaidi Ulaya.

Cha kushangaza rekodi hiyo inashikiwa na nyota wa kimataifa wa Ufaransa, Bafetimbi Gomis. Mchezaji huyo aliweka rekodi hiyo mwaka  2011 wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Olympique Lyon na Dinamo Zagreb ya Croatia.

Gomis, 33, alifunga mabao matatu chini ya dakika 10 na kuisaidia Lyon kuweka rekodi ya ushindi mkubwa. Hakuna mchezaji hadi sasa aliyeweza kutupia hat-trick ya mapema kama yeye kwenye michuano hiyo ya Uefa.