Shule ya Lake Baba yafanya mahafali ya 11 tangu kuanzishwa

Na John Walter-Babati

Wazazi na walezi wametakiwa kuwasaidia watoto wao  pindi wanatakaporudi nyumbani kusubiri matokeo ya kidato cha nne na sio kuwaozesha ili waweze kufikia ndoto zao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji  wa wilaya ya Babati Hamisi Malinga alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lake Babati katika mahafali ya 11 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka .

Malinga amesema ni jukumu la kila mzazi/mlezi kuhakikisha  watoto wao wanaepuka vitendo vitakavyosababisha kukatisha ndoto za wanafunzi hao pindi  wanaporejea nyumbani baada ya mitihani yao ya mwisho.

Amesema katika halmashauri yake atahakikisha watu  wenye tabia za kuwadanyanya wanafunzi kwa namna moja ama nyingine  wanachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari   Lake Babati  iliyopo mjini Babati mkoani Manyara, Lenadi Mao amewataka Walimu, Wanafunzi na Wafanyakazi katika taasisi za elimu nchini  kuzingatia nidhamu shuleni ili kuweza kuchochea maendeleo ya ufaulu kwenye shule zao.

 Katika mahafali hayo  ya 11 ya kidato cha nne ya shule hiyo yalienda sambamba na harambee ndogo kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana na wavulana shuleni hapo .

Mao alisema licha ya kuwa wanayo mabweni, wamedhamiria kuongeza mengine mawili  ili kuwanusuru wanafunzi na vishawishi huko mitaani vitakavyoweza kuwaharibia masomo yao.

Ameeleza kuwa mabweni hayo mpaka kukamilika yatagharimu kiasi cha shilingi milioni hamsini za kitanzania na wanatarajia kukamilisha ujenzi huo muhula mpya wa masomo January 2019.

Mao amesema pamoja na hayo shule yake imelipa kipa umbele zaidi suala la nidhamu muda wote   kwa  walimu na wafanyakazi ili kuchochea maendeleo ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo.

“Nidhamu si kwa wanafunzi pekee bali inatakiwa kuanzia hata kwangu mimi mkurugenzi  wa shule pamoja na walimu na wafanyakazi wengine katika shule yetu hii, hivyo kwa mwalimu anayefanya kazi hapa kwenye mkataba anasaini nidhamu, ” alisema Mao.

Alisema nidhamu inapoanzia kwa viongozi wa juu, walimu na wafanyakazi wengine inasaidia nidhamu hiyo hiyo kuingia hadi kwa wanafunzi ambayo inawachochea kufanya vizuri katika masomo yao darasani.

Aidha Mkurugenzi huyo, aliwataka wahimu hao wa kidato cha nne kuzingatia nidhamu mahali popote watakapokuwa mara baada ya kutoka shuleni hapo kwa faida yao  huko waendako.

Mao alisema nidhamu ndiyo siri ya mafanikio ya shule hiyo katika ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo kwani wamekuwa wakiwafunisha ukakamavu kupitia kwa vijana wa Skauti na kuongeza kuwa ni vyema wahitimu hao wa kidato cha nne wakaendeleza nidhamu waliyokuwa wakiionyesha shuleni hapo huko wanapokwenda ili iweze kuwasaidia katika maisha yao ya baadae.

Aliongeza kwa kuwataka wazazi wanaopeleka watoto wao katika shule hiyo kuwa na amani muda wote  kutokana na kwamba wapo katika mikono salama wakilelewa kimwili na kiroho.