Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka Watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuhakikisha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanahudumiwa vizuri kwa kupata ruzuku zao kwa wakati ili kuziwezesha kaya hizo kujikimu kimaisha na kuondokana na umaskini.
Dkt. Mwanjelwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa TASAF makao makuu katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya TASAF na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.
kwa kuwahudumia vizuri wanufaika hao, TASAF pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itapata baraka za Mwenyezi Mungu ambaye kupitia vitabu vyake vitakatifu ameelekeza kuwasaidia maskini na pia watakuwa mfano bora wa kuigwa na nchini nyingine barani Afrika kwa kutekeleza vema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameitaka TASAF kuhakikisha inaweka taratibu madhubuti za kisheria zitakazowaadhibu na kuwadhibiti wote watakaobainika kufanya udanganyifu kujipatia fedha za mpango wakati hawana sifa za kuwa wanufaika, lengo likiwa ni kujenga nidhamu katika jamii ili fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ziwafikie walengwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anavyotaka.
