Kamati ya Bunge ya Bajeti yatembelea kiwanda cha kutengeneza Transfoma


Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge la bajeti George Simbachawene ameambatana na wajumbe wake kutembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC kilichoko jijini Arusha ili kukagua masuala mbalimbali hususani uwezo wake katika uzalishaji wa transfoma ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na vifaa vya umeme vya kutosha.

Aidha katika ziara hiyo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wajumbe hao kwa nyakati tofauti waliwapongeza watendaji wa Kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma nyingi ambazo ni 14,000  kwa mwaka huku mahitaji ya transfoma nchini kwa mwaka yakiwa ni 10,000.

Vilevile Wajumbe walienda mbali zaidi na kupongeza uamuzi wa Serikali wa mwaka 2017 ambao ulielekeza kuwa miradi yote ya umeme nchini itumie vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini hali inayopelekea miradi hiyo kutekelezwa kwa kasi.

Halikadhalika walimtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kuwa mbunifu kwa kuangalia pia masoko mengine ya transfoma na si kulenga miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.

Awali, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa, Serikali ilichukua uamuzi wa kusitisha kuagiza nje vifaa vya umeme vinavyopatikana nchini ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.
Mpya zaidi Nzee zaidi