Wizara kuandaa mikakati ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria


Na Thabit Hamidu,Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sulueiman amesema Wizara yake itaendelea kutumia mikakati ya kupambana na malaria ambayo imeonyesha mafanikio makubwa ya kupunguza maradhi hayo ili kuhakikisha maradhi hayo yanaondoka kabisa.

Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kutumia tiba ya dawa mchanganyiko, kufanya ufuatiliaji wagonjwa majumbani na kuendeleza zoezi la upigaji dawa majumbani katika sehemu ambazo bado wagonjwa wa maradhi hayo wanapatikana.

Naibu Waziri ameeleza hayo katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa mpira wa Misuka, Mahonda Wilaya ya Kaskazini B.

Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kupambana na malaria hadi kufikia chini ya asilimia moja lakini bado kuna baadhi ya sehemu hasa katika Wilaya Kaskazini B, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Magharibi bado maradhi hayo yapo.

Pia alieleza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ikishirikiana na wadau mbali mbali zikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa za ndani na nje ya nchi.

Aidha aliwataka wananchi waliopata vyandarua waendelee kuvitumia kikamilifu pamoja na kuvitunza kwani kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wagonjwa majumbani unaonyesha kuwa matumizi ya vyandarua kwa jamii bado yapo chini.

Aliweka Wazi kuwa Wizara ya Afya itaendelea kutoa vyandarua bila malipo kupitia vituo vya afya kwa mama wajawazito , watoto wenye umri wa miezi tisa na wanajamii kwa jumla.

Aliwakumbusha wananchi kuwa huduma za uchunguzi wa malaria zinapatikana katika vituo vyote vya afya, vikiwemo vituo vya bandarini na uwanja wa ndege ambavyo vimewekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na kutoka Zanzibar.

Akizungumzia hali ya Malaria katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Katibu Tawala Wilaya Kaskazini ‘B’ Makame Machano alisema jumla ya watu 52,356 waliochunguzwa mwaka jana, watu 655 sawa na asilimia 1.3 walibainika kuwa na vimelea vya Malaria na wengi wanatoka Wilaya ya Kaskazini B.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani kwa upande wa Zanzibar mwaka huu ‘‘Zanzibar bila Malaria inawezekana’’. ‘Mimi na wewe tumalize Malaria Zanzibar’.