Marubani wanafunzi wa Afrika Kusini, waliotengeneza ndege aina ya Sling 4, wamewasili mkoani Kilimanjaro, wakiwa njiani kuelekea kwenye kituo chao cha mwisho jijini Cairo, Misri.
Timu ya wanafunzi hao iliondoka Zanzibar jana Jumapili, baada ya kutumia siku kadhaa wakiwa katika mazungumza na mamlaka za nchini Kenya ili waweze kupata ruhusa ya kutua jijini Nairobi, mazungumzo ambayo hayajazaa matunda.
''Mamlaka nchini Kenya wamesema hawajafurahishwa na njia zetu hivyo wametuzuia kuingia,'' alisema kiongozi wa wanafunzi hao, Des Werner, Baba wa Megan Werner 17, mwanzilishi wa U-Dream Global.
''Tunaweza kubadili njia lakini hatuna muda wa kufanya hivyo.Tunafikiri kama ni wagumu tusilazimishe kwenda. Hata hivyo ni nchi yao ndiyo inayokosa nafasi ya vijana wa nchini kwao kuzungumza na timu yetu kwaajili ya kuwapa msukumo vijana wa nchini mwao.'' aliongeza.