Faida za kutumia mbolea ya samadi

Samadi ni aina ya mbolea ambayo hutokana na vinyesi vya wanyama mbalimbali kama ng’ombe, kuku, mbuzi, kondoo na wengine. Hii ni miongoni mwa mbolea ambazo wakulima wengi wanaweza kumudu kirahisi.

Vilevile mbolea zingine ambazo wakulima wanaweza kuzipata kwa urahisi ni masalio ya mimea shambani (mabiwi). Mfano wa masalio hayo ni kama mabua ya mtama, mahindi na mimea ya jamii ya kunde au kitaalamu hujulikana kama (leguminas). Masalio haya yakishaoza hurutubisha udongo kwa kurejesha chumvichumvi za madini zilizokuwa zimechukuliwa na mimea wakati inastawi.

Hata hivyo mbolea yenye manufaa zaidi ni samadi, kwani wataalamu wanakadiria kuwa tani moja ya vinyesi vya fahali (madume ya ng’ombe) huwa na thamani karibu kilo 6.3 za chumvichumvi za nitrates; tani moja ya samadi ya vinyesi vya ng’ombe majike huwa na kilo 5.1 za chumvi za nitrates.

Mbolea zinazotokana na masalio ya mimea kwa mfano, mabua ya mahindi tani moja hutoa mbolea inayoweza kurejesha ardhini karibu kilo 4.0 za chumvi za nitrates.

Hivyo samadi yenye mchanganyiko wa vinyesi vya ng’ombe majike na madume wanaofugwa kwa pamoja (wanaolala katika zizi moja) huwa na thamani kubwa.

Ili upate kustawi na kutoa mavuno mengi na bora, mimea huhitaji chumvichumvi za madini ya nitrates, phosphate na potash pamoja na kiasi kidogo sana cha chumvi za nitrates, phosphate na potash pamoja na madini ya boron, copper, manganese, zinc na nyinginezo.

Kwa hiyo rutuba ya udongo huwa inategemea sana kiasi cha chumvichumvi zilizomo udongoni.

Ubora wa samadi hukadiriwa pia kwa kiasi cha chumvi za madini zinazopatikana mathalani ng’ombe 50 wanaweza kutoa karibu tani 600 za samadi kila mwaka. Kiasi hiki cha samadi kinaweza kurejesha ardhini karibu kilo 3048 za chumvichumvi za nitrates, kilo 544 za phosphate na kilo 2722 za Potash, pamoja na kiasi kidogo cha Boron, Copper, Manganese na Zinc.

Wakulima au wafugaji wengi hufuga ng’ombe hata zaidi ya 50, lakini kwa wastani wengi huwa na idadi hiyo kama ni wastani wa ng’ombe ambao kila mkulima anaweza kuwa nao.

Mbolea yenye kilo 3048 za nitrates, kilo 544 za phosphate na kilo 2722 za potash kwa uwiano huo haziwezi kutengenezwa kiwandani kwani itakuwa ghali sana kiasi kwamba hakuna mkulima anaweza kununua.

Samadi kiasi hicho italeta manufaa mengi kwani licha ya kuongeza rutuba ardhini vilevile itaubadili udongo uwe katika hali nzuri zaidi kwa kustawisha mimea.

Kadhalika samadi unaufanya udongo ushikamane kwa nguvu zaidi hata usiweze kupeperushwa na upepo au kumomonyolewa na maji ya mvua.

Manufaa mengine ya mbolea ya samadi ni kuwa inaufanya udongo kuwa katika hali nzuri ya kuweza kuyashikilia maji au unyevu kwa muda mrefu.

Minyoo waishio udongoni ambao husababisha kuwepo nafasi kwa ajili ya hewa kupenya kwa urahisi na vijidudu vya bakteria ambavyo huozesha mbolea na kubadili hewa kuwa katika hali ya chumvichumvi zinazotumiwa na mimea, hupata mazingira mazuri kwa maisha yao katika udongo uliotiwa samadi.

Wataalamu wanasema kuwa ubora wa samadi inategemea jinsi ilivyokuwa imetunzwa zizini au kibandani kwani chumvi nyingi hasa zile za nitrates huwa zinapotea kwa urahisi kwa maji ya mvua, kutokana na kitendo chake cha kuyeyuka mara tu zinapolowa maji.

Ili tuendelee kuwa na thamadi kubwa ni muhimu zizi liwe na paa lisilovuja kusudi maji ya mvua yasilowanishe, la sivyo ng’ombe wafugwe katika vibanda.