Mahakama Kuu ya Tanzania leo imeanza kusikiliza hoja za Tundu Lissu alizoziwasilisha mahakamani kupinga kuvuliwa ubunge na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai huku upande wa utetezi ukizipinga.
Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.
Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Spika Ndugai awasilishe mahakama taarifa ya kumvua ubunge, aliyoitoa bungeni ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.
Nyingine ni Mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu, wa Chama cha Mapinduzi.
Maombi hayo yametajwa leo Alhamisi Agosti 15,2019 na mawakili wa Lissu wakiomba mwongozo wa mahakama ili waweze kuzungumzia ombi la kusimamishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, lakini ombi hilo limepingwa na mawakili wa Serikali wakidai kwa sasa sio muda muafaka wa kuanza kulisikiliza.
