Msemaji Mkuu wa Serikali aifunda TRC kuhusu kuutangaza mradi ya Reli SGR


Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi ametoa mafunzo kwa watumishi wa Shirika la Reli Tanzania TRC kuhusu umuhimu wa mawasiliano kimkakati katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.

Katika mafunzo hayo, Dkt.Abbasi amesema kuwa ili miradi mikubwa iweze kujulikana kwa wananchi, Taasisi husika zinapaswa kuzingatia misingi mikubwa minne katika kuandaa habari ili kuwahabarisha wananchi kuhusu miradi hiyo, akakumbusha;

Katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, Serikali ilitoa Fedha za utekelezaji wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) ambapo TRC inapaswa kutangaza mradi kwa wananchi, akasema, “kuna misingi minne ambayo inapaswa kutekelezwa ili kuwezesha mawasiliano ya kimkakati katika mradi huo ambao wananchi wanapaswa waujue,” Dkt.Abbasi.

Msemaji Mkuu huyo wa Serikali aliitaja misingi hiyo kuwa ni Maono katika kuwahabarisha wananchi (Pro-Active), akaeleza kuwa ili wananchi waweze kujua kinachoendelea katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), TRC ambayo inakabidhiwa fedha nyingi za walipa kodi,haina budi kuonesha zinavyotumika.


Msingi mwingine Dk. Abbasi ametaja kuwa ni Ujumbe unaotolewa (Messaging) katika kutekeleza kufikisha ujumbe kwa wananchi, akasema, TRC inapaswa kuwaeleza wananchi kwa mahususi kuhusu mradi huo kuwa utakuwa na manufaa na faida gani kwa fedha zao.


Akaongeza kuwa katika kuutangaza maradi huo, TRC wanapswa kuwa na mawasiliano baina ya wao na taasisi au wadau wao (Collaborations) ili hatimaye kubainisha kwa wananchi wayasemayo ili kuwezesha upatikanaji wa habari sahihi, hapa alisema wataalum katika kada mbalimbali kwenye Taasisi wanapaswa kushiriki kimkakati kutoa takwimu za kitaalamu kwa Afisa Habari ili aweze kuzinyambua kabla ya kuzipeleka kwa wananchi au walengwa.

Alitaja msingi mwingine ni kuweza kutanua wigo kwa kutumia Vyombo mbalimbali Kuhabarisha (Multi-Media) hii ni dhana ya kutumia njia nyingi za habari, kuhabarisha wananchi hasa mitandao ya kijamii,magazeti, radi na runinga, na kuwatumia wataalum wa kada ya Habari kwa kuandaa picha, Video na Graphics, kuandika habari na makala ili kurahisisha mtazamaji au msomaji kuelewa haraka kwa njia hizo na hivyo kuuelewa mradi wa SRG.

“Taasisi za Serikali mnapaswa kuwekeza zaidi kwenye kitengo cha habari, ikiwemo kuwa na wataalamu mbalimbali katika kada hii, lakini mnatakiwa muwe hasa kwenye mitandao ya kijamii”

Akaeleza kuwa nusu ya watu duniani wako kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa, na kwamba jitihada zinaendelea za kubadilisha Taasisi mbalimbali kutoka kutegemea gazeti la kesho badala ya pia kutumia mitandao ya kijamii ambako taarifa zinafika kwa haraka na kwa uhakika zaidi kwa watu wengi.

Aidha, Dkt. Abbasi alitembelea ujenzi wa Stesheni mpya ya reli ya kisasa SGR ambapo alielezwa ujenzi wa reli unaendelea vizuri, na akawataka watanzania kuiunga mkono Serikali ili kutekeleza kwa pamoja ujenzi wa Reli hiyo na akasema,”reli hii itakuwa na manufaa kwa vizazi vya leo, kesho na vijavyo”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu waTRC, Masanja Kadogosa alisema kuwa katika kutekeleza masuala ya kuwajuza wananchi kuhusu mradi huo, Idara ya Habari ni muhimu na amemshukuru Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO kuwatembelea na kuwapa darasa katika masuala ya mawasiliano kimkakati kwenye mradi wa SGR.

“Siku zote tunasema huu ni mradi mkubwa sana ambao Serikali inautekeleza ndani ya nchi yetu, na wananchi hawa wakati wote wanahitaji kuhabarishwa manufaa ya mradi huu, kwa hiyo ujio wa Msemaji Mkuu wa Serikali kwetu sisi ni faraja ya kupata uzoefu mkubwa kwenye masuala ya Habari”, alisema Kadogosa.