Dk. Leonard Maboko, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), amesema Watanzania wasijisahau kwa sababu Ukimwi upo na takwimu za maambukizi mapya zinaonesha kwamba watu 72,000 wanaambukizwa kwa mwaka.
Alitoa kauli hiyo baada ya kutembelea kijiji cha Lupeta, Kata ya Lupeta wilayani Mpwapwa, katika mkoa wa Dodoma na kuzungumza na wasichana na wanawake wanaosaidiwa fedha na taulo za kike kupitia mradi wa Timiza Malengo.
Dk Maboko alisema kutokana na takwimu hizo, watu 6,000 wanapata maambukizi mapya katika kila mwezi, hivyo kwa mwezi mmoja wanaambukizwa watu 200.
"Maambukizi hayo mapya ni makubwa miongoni mwa vijana wa umri wa miaka ya kati ya 15 na 24, ambapo vijana wa umri huo wanaambukizwa kwa asilimia 40 kati ya maambukizi mapya yote,"alisema.
Dk Maboko alisema kitu kibaya zaidi kati ya vijana hao 80 wasichana ni 64, na 16 wanaobaki ni wavulana. Hiyo ina maana kwamba kati ya vijana 10 wanaoambukizwa maambukizi mapya kwa siku, wanane ni wasichana na wavulana ni wawili.
Dk Maboko alisema kutokana na takwimu hizo, mradi huo wa majaribio wa Timiza Malengo umelenda kusaidia wasichana na wanawake hasa wa mazingira magumu ili kuwasaidia kupata Sh 50,000 kila mwezi na taulo za kike nne kila mwezi.
Alisema mradi huo ambao unalenga wasichana waliopo shuleni hasa wanaotoka katika mazingira magumu, unakusudia kupanuka na kwenda kwa wasichana waliopo katika mazingira magumu nje ya shule.
