ATCL ipo tayari kumsafirisha bure anayepumulia mashine


 ATCL (Shirika la Ndege Tanzania) limesema lipo tayari kumlipia gharama za usafiri mgonjwa anayepumulia mashine, Hamad Awadh (28) kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mumbai, India.

Shirika hilo litatoa tiketi mbili za ndege kwenda India na kurudi Tanzania kutibiwa.

Hayo yameelezwa ikiwa zimepita siku tano tangu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuahidi kutoa Sh11.5 milioni, Sh10 milioni zikiwa kwa ajili ya matibabu na Sh1.5 milioni kumsaidia gharama za umeme.

Akizungumza na mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema watagharamia usafiri wa kwenda na kurudi.

“Tumempatia masharti yetu kwa kuwa ATCL inakwenda Mumbai India, tutamsafirisha iwapo atapata hospitali iliyopo Mumbai ili iwe rahisi kwake katika usafiri kwa maana tutamfikisha pale na tutaweza kumrudisha bila shida yoyote kwa gharama zetu,” amesema Matindi.