Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni mia tano(500) kwa ajiri ya kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri Madaba sambamba na kuendelea kuboresha zahanati za Mbangamawe na Magingo ili kukidhi hadhi kuwa vituo vya afya.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Josephat Kandege, bungeni wakati akijibu, swali la Mbunge wa jimbo la Madaba, Joseph Mhagama, aliyehoji ni lini serikali itazipandisha hadhi zahanati za Mbangamawe na Magingo kuwa vituo vya afya kama alivyoahidi waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa ziarani Wilayani humo.
Naibu waziri Kandege, amesema tayari serikali imeshatenga kiasi cha shilingi milioni mia tano(500) tayari kuanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Madaba, pia imetenga milioni 120 kwa ajili ya ukarabati wa zahanati ya Mbangamawe, na milioni mia moja(100) kwa ajili ya zahanati ya Magingo.
“katika kuendelea kuboresha huduma za afya Madaba katika mwaka wa fedha 2019/2020, serikali tumetenga kiasi cha shilingi million mia tano(500) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Madaba, na itaendelea na jitihada za kujenga , kukarabati, kupanua na kuboresha miondombinu ya afya Madaba”amesema Kandege.
Pia amebainisha kuwa katika tathmini iliyofanyika imebaini kuwa ujenzi wa zahanati zote mbili umefika asilimia 45, na kila zahanati inajengo moja kubwa lenye vyumba 21 kwa kufuata ramani zilizotolewa na Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto kabla ya 2010, pindi upanuzi utakapo kamilika vitapandishwa hadhi kuwa vituo vya afya.
