Wahudumu wa meli ya mafuta ya Uingereza kuachiliwa Iran


Iran itawaachilia wahudumu saba wa meli ya mafuta wanayoishikilia yenye bendera ya Uingereza Stena Impero.

Hayo yameripotiwa leo na kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya Iran. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje Abbas Mousavi amekiambia kituo hicho kuwa wahudumu hao ambao miongoni mwao ni raia wa India waliruhusiwa kuondoka kwenye meli hiyo kwa misingi ya kiutu.

Meli hiyo kwa jina Stena Impero inayomilikiwa na Sweden, ilikamatwa na askari wa kikosi cha mapinduzi wa Iran Julai 19, katika Mlango bahari wa Hormuz, kufuatia madai kuwa ilikiuka sheria za usafiri wa baharini.

Hayo yalijiri wiki mbili baada ya Uingereza kuikamata meli ya mafuta ya Iran katika pwani ya Gibraltar.

Kukamatwa kwa meli ya Iran kulizidisha mzozo kati ya Tehran na nchi za magharibi, tangu Marekani ilipojiondoa katika mkataba wa nyuklia mwaka uliopita.
Mpya zaidi Nzee zaidi