Na Ahmad Mmow, Lindi.
Mmoja wa wanufaika wa shirika la msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto wa Lindi( LIWOPAC), Rose Wangubo ametoa wito kwa wanaolalamika ugumu wa maisha wafanye kazi kwa juhudi na maarifa ili waondokane na hali hiyo.
Wangubo aliyasema hayo kijijini Mnara, jana alipozungumza na Muungwana Blog baada ya kumtembelea ili kuona mafanikio yaliyopatikana baada ya wasaidizi wa kisheria wa LIWOPAC kumsaidia kupata mashamba na vyombo vya ndani kutoka kwa aliyekuwa mume wake Rose ambae pia alitoa wito kwawanawake wanaoteswa na kunyanyaswa na waume zao waache kulia na kukata tamaa, alisema wanaoilaumu serikali kutokana na ugumu wa maisha wanaitwisha lawama isiyostahili.
Kwani hakuna serikali inayoweza kugawa fedha taslimu kwa kila mtu. Bali njia ya kuondokana na ugumu wa maisha nikufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Alisema yeye baada ya kufanikiwa kupata shamba kutoka kwa aliyekuwa mumewe aliyeishi nae kwa miaka 19, lakini alikataa kumgawia kitu chochote hadi wasaidizi wa kisheria walipomsaidia na kufanikiwa kupata mashamba na vyombo vya ndani anaimani kuwa ni miongoni mwa watakao miliki nyumba ya kisasa na gari ndani ya miaka kumi kutoka sasa.
'' Baada ya kupata shamba nikaamua kupanda miti. Nipanda miti 200 na bado nampango wa kuendelea kupanda, lakini tatizo ni mtaji. Ninauhakika wanaonibeza kwakusema nitazeeka na kupoteza ujana wangu kwakufanyakazi muda mwingi, watapata majibu kwa vitendo,'' alisema Wangubo.
Alibainisha kwamba familia nyingi ni maskini kwasababu ya watu kushindwa kupanga na kusimamia kikamilifu mipango ya muda mrefu ya maendeleo. Hali ambayo inasababisha warithishe umaskini kwa watoto wao.
Alisema nijambo la aibu mtu aliyetimia viungo na mwenye afya njema kulia umaskini na ugumu wa maisha wakati kunafursa nyingi zinazoweza kumfanya asiwe maskini. '' Yule baba( Rais Dkt John Magufuli) nampenda sana, anasema kweli nchi hii nitajiri bali watu tunashindwa kumuelewa baba wa watu yule. Umaskini unasababishwa nasisi wenyewe sio serikali.
Mtu unamiguu na mikono na akili timamu unaacha kufanyakazi unasema Rais amebana hela, amebana kwakoleo au supana?,'' alihoji Wangubo.
Mwanamke huyo alisema baadhi ya watu, akiwamo yeye wamerithi umaskini wa wazazi wao ambao kushindwa kupanga mipango ya muda mrefu.
Akisema kwamba hata sasa wapo wanaoshindwa kupanda mazao yanayochukua muda mrefu kabla yakuanza kuvunwa kwamadai kwamba watakufa kabla kuanza kuvuna. Mawazo ambayo hayafai kuwepo kwa wapenda maendeleo.
Aidha Wangubo alitoa wito kwa wanawake wanaoteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa na waume zao wasikate tamaa na kuanza kulia. Bali wapiganie haki zao bila kuchoka. Kwani yeye aliposhindwa kupambana peke yake alikwenda mahakamani akasaidiwa akajengewa nyumba na aliyekuwa mume wake. Huku LIWOPAC wakimsaidia kupata mashamba ambayo siku hadi siku yanabadilisha maisha yake.
'' Wanawake wanaokimbilia mijini wajue umaskini hausababishwi na vijiji bali fikra zao. Watajuta watakapo rudi vijijini nakukuta ardhi imekwisha. Tulio vijijini tupange ratiba za kazi ambazo zitatufanya tukose muda wakukaa na kufanya umbea,'' Rose alitupa kijembe kwa wapenda makundi ya umbeya badala ya maendeleo.
