Baba amuua mwanae wa miaka miwili kwa kumchoma na moto

Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia Juma Daniel, mkazi wa Kijiji cha Kazingati kata ya Keza wilayani Ngara, kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kumzaa, mwenye umri wa miaka miwili.

Daniel anadaiwa kumuuwa mwanaye huyo kwa kumchoma moto usoni na makalioni na kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali sehemu za haja kubwa, baada ya mtoto huyo kujisaidia haja kubwa kitandani wakati wamelala.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, amesema kuwa Baba huyo alikwishatengana na mama mzazi wa mtoto huyo na kuoa mke mwingine.

Aidha Kamanda Malimi alilitaja jina la mtoto huyo kuwa ni Bahati Juma, na kwamba alifanyiwa kitendo hicho cha kikatili Disemba 27, 2019 na hakupelekwa hospitali badala yake alianza kumtibu kienyeji nyumbani, na baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya baba huyo alitoroka.