Nchi tatu za Ulaya zaanza mchakato wa kuiwajibisha Iran

Nchi tatu za Umoja wa Ulaya zimekitumia kipengele cha kusuluhisha mizozo katika makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, yaliyosainiwa mwaka 2015.

Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ambazo zimeyatia saini makubaliano hayo, zimesema zimechukua hatua hiyo baada Iran kukiuka mara kwa mara ukomo wa kurutubisha madini ya urani uliowekwa katika makubaliano hayo.

Hata hivyo nchi hizo za Ulaya zimesisitiza kwa mara nyingine kuwa zinaendelea kuyaunga mkono makubaliano hayo, zikipinga shinikizo la utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kuzitaka kuyatupa mkono.

Marekani ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka jana, na kurejesha vikwazo vilivyokuwa vimelegezwa dhidi ya Iran.

Uamuzi huo wa Marekani umeongeza joto la mvutano kati yake na Iran, ambao ulikaribia kuingia katika vita kamili baada ya Marekani kumuuwa jenerali maarufu wa Iran, Qasem Soleimani, mwanzoni mwa mwezi huu.