Na John Walter, Babati.
Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini (CCM) Mheshimiwa Paulina Gekul ametoa wito kwa wakazi wa mji wa Babati kutumia fursa mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali na biashara ili kujijengea uwezo wa kujiamini pale wanapoamua kujihusisha na biashara.
Ametoa wito huo akiwa kwenye mafunzo aliyoyaandaa kwa ajili ya wakazi wa jimbo la Babati mjini kuhusu ujasiriamali na biashara yaliyoanza leo jumatano februari 27 katika ukumbi wa Ccm babati mjini.
Amesema kwa kuwa mjini hakuna shughuli za kilimo hivyo semina hiyo itafungua njia kwa wale wanaotarajia kuanzisha biashara zao na kufanya shuguli za ujasiriamali.
Amesema semina hiyo ambayo inafanyika kwa siku tatu bila malipo katika ukumbi wa mikutano wa Ccm mjini Babati, itawasaidia wanawake na vijana kujiajiri wenyewe.
Amesema mafunzo ya ujasiriamali na biashara ni nguzo muhimu kwa vijana na Wanawake hasa wanapokuwa na malengo ya kujiajiri kwani mafunzo hutoa mwongozo.
Mbunge huyo amesema semina hiyo ameileta kwa kuonyesha upendo alionao kwa wananchi wake huku akiwaleta wataalamu kutoka sehemu mbalimbali ambao wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa nadharia na vitendo.
Aidha amewataka wananchi wote wa Babati wajitokeze kwa wingi kupata mafunzo hayo ambayo yanatolewa bila malipo kuanzia leo februari 27,2020 hadi februari 29.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Simon Lulu amempongeza Mbunge Gekul kwa jitihada za kuwakutanisha vijana na wanawake pamoja na kutoa mafuzo hayo ya ujasiriamali na biashara.