Na John Walter, Manyara.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Mheshimiwa Simon Lulu amewataka wananchi wampigie kampeni bila uoga Rais John Magufuli kwa kuwa chama hakina mpango wa kumsimamisha mgombea mwingine.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Babati waliohudhuria katika semina ya ujasiriamali iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Babati mjini Paulina Gekul katika ukumbi wa mikutano wa Ccm, alisema mambo anayoyafanya Rais Dk Magufuli ni mazuri na yanalipeleka Taifa mbele.
Amesema kama si matakwa ya Katiba ya nchi, uongozi wa Rais John Magufuli ulipaswa kuendelea kuwapo miaka yote.
Amesema laiti ingelikuwa Katiba iliyopo haikufupisha muda wa uongozi wa rais, angeshauri Rais Dk Magufuli awe Rais wa Tanzania wa siku zote.
Amesema Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa Mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla katika afya,elimu na miundo mbinu.
Aidha amesema kuhusu Madiwani na Wabunge hilo litapangwa na ndani ya chama hivyo wananchi wasubiri “ila kuhusu rais hakuna swali”.
Simon aliwataka wanaopatiwa mafunzo hayo wakayatumie vizuri katika kujiinua kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.
